Michezo

Pogba ataka Manchester United wamlipe Sh78m kwa wiki

October 7th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

MINO Raiola ambaye ni wakala wa kiungo Paul Pogba amedokeza kuhusu uwezekano wa nyota huyo mzawa wa Ufaransa kubanduka uwanjani Old Trafford mwanzoni mwa Januari 2020 iwapo Manchester United watashindwa kumlipa kiasi cha Sh78 milioni kwa wiki.

Pogba ambaye angali na miaka miwili katika mkataba wake na Man-United, hakuwa sehemu ya kikosi cha waajiri wake kilichochuana na Newcastle United katika kipute cha EPL Jumapili uwanjani St James Park.

Kwa upande wao, Man-United wamesisitiza kwamba hawana pupa yoyote ya kurefusha mkataba wa Pogba ambaye alikuwa sehemu muhimu zaidi katika kampeni za Ufaransa waliotawazwa mabingwa wa fainali za Kombe la Dunia zilizoandaliwa Urusi mnamo 2018.

Iwapo Man-United watampokeza Pogba mkataba mpya kwa malipo ya hadi Sh78 milioni kwa wiki jinsi anavyodai wakala wa sogora huyo wa zamani wa Juventus, basi atakuwa amekifikia kiwango cha nyota Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wa Barcelona na Juventus mtawalia.

Ingawa vinara wa Man-United wamekiri kwamba hawajaanzisha mazungumzo yoyote ya kujadili mustakabali wa Pogba, kubwa zaidi katika maazimio yao ni kumdumisha kiungo huyo ugani Old Trafford licha ya maarifa yake kuwaniwa pakubwa na Real Madrid na Barcelona.

“Lengo kuu la Pogba kwa sasa ni kurejea katika hali shwari itakayomwezesha kuwatambisha Man-United katika kampeni zote za muhula huu. Tetesi kwamba ametupa masharti mapya kuhusu mshahara wake hazina mashiko,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa jana na Man-United na kunukuliwa na gazeti la Mirror Sport.

Pogba ameachwa na kocha Didier Deschamps wa timu ya taifa ya Ufaransa nje ya kikosi atakachokitegemea kuvaana na Albania na Andorra katika michuano ijayo ya kufuzu kwa fainali za Euro 2020.

Ni matarajio ya Man-United kuwa nyota huyu atakuwa katika fomu nzuri ya kutisha zaidi watakapokuwa wenyeji wa Liverpool katika kivumbi cha EPL kitakachowakutanisha uwanjani Old Trafford mnamo Oktoba 20, 2019.

Mnamo Julai 2019 kocha Zinedine Zidane wa Real Madrid alikitaka kikosi hicho kujinasia huduma za Pogba.

Ingawa hivyo, mpango huo uligonga ukuta baada ya Rais Florentino Perez aliyetumia zaidi ya Sh33 bilioni kuisuka upya klabu hiyo kukataa kufungulia zaidi mifereji yake ya pesa.

Kiini cha Zidane kufufua juhudi za kuwania huduma za Pogba ni ubaya wa jeraha la goti ambalo kiungo Marco Asensio alipata wakati wa mchuano wa kujifua kwa msimu mpya uliowakutanisha na Arsenal.

Pogba ambaye aliwagharimu Man-United kiasi cha Sh12 bilioni kutoka Juventus mnamo 2016, aliwahi pia kudokeza uwezekano wa kurejea Juventus, Italia.