Michezo

Pogba augua Covid-19

August 28th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO matata wa Manchester United, Paul Pogba, 27, amepatikana na virusi vya corona.

Haya ni kwa mujibu wa kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps.

Pogba kwa sasa atajitenga kwa siku 14 zijazo.

Ina maana kwamba nyota huyo wa zamani wa Juventus hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Deschamps katika mechi ya Uefa Nations League dhidi ya Uswidi mnamo Septemba 5 ugenini kisha ile itakayowakutanisha na Croatia jijini Paris siku tatu baadaye.

Hata hivyo, Pogba atakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuwajibishwa na Man-United watakapofungua rasmi kampeni zao za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2020-21 dhidi ya Crystal Palace. Mechi hiyo itachezewa uwanjani Old Trafford mnamo Septemba 19.

“Kila mmoja kambini mwa Man-United anamtakia Pogba afueni ya haraka kadri kikosi kinavyojiandaa kwa msimu mpya,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Man-United.

Nafasi ya Pogba katika kikosi cha Ufaransa sasa itatwaliwa na chipukizi mahiri wa Rennes, Eduardo Camavinga, 17.

“Nimekifanyia kikosi change cha Ufaransa mabadiliko muhimu katika kipindi cha mwisho. Nafasi ya Pogba kwa sasa inachukuliwa na Camavinga,” akasema Deschamps.