Michezo

Pogba awataka 'Mashetani Wekundu' waitie Barcelona adabu

April 14th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

KIUNGO wa Manchester United Paul Pogba amesema timu hiyo lazima ijiimarishe iwapo inalenga kuibandua Barcelona kwenye mechi ya robo fainali ya Klabu Bingwa Barani Uropa (UEFA) Jumanne ya Aprili 16.

Mchuano wa mkondo wa kwanza kati ya timu hizi uliishia 1-0 kwa manufaa ya Barcelona Jumatano Aprili 10 ugani Old Trafford.

Pogba ambaye taarifa zinaendelea kudai yupo njiani kuhamia Real Madrid ya Uhispania, alieleza kusikitishwa na jinsi Manchester United ilivyosakata gozi kwenye ushindi wa 2-1 dhidi ya West Ham katika Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) ugani Old Trafford Jumamosi Aprili 15.

“Kwa hakika hatukucheza vizuri ingawa tumepata ushindi. Mechi ilikuwa wazi japo hatukutumia nafasi zetu vizuri na tukacheza kwa mwendo wa kobe. Lazima tuimarishe uchezaji wetu iwapo tunalenga kupiga hatua.

“Siwezi kueleza iwapo hayo yalisababishwa na uchovu baada ya kupambana na Barcelona. Wacha tupumzike kabla ya kuvaana na Barcelona siku ya Jumanne,” akasema Pogba.

Akigusia penalti mbili alizofunga katika dakika ya 19 na 80, Mfaransa huyo alifichua kuwa siri yake ya kuchanja mikwaju ya penalti kwa ustadi ni kuangalia mahali wanyakaji husimama.

“Pengine nilimbwaga kipa kisha nikaujaza mpira wavuni. Hats hivyo tulikuwa na bahati na tukapata alama zote tatu. Lazima tujiimarishe kuipiga Barcelona,” akaongeza Pogba.