Michezo

Pogba kupokezwa 'hongo' ya unahodha asihamie Real Madrid

April 14th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

KAMA njia ya kumshawishi asalie ugani Old Trafford, duru zinaarifu kwamba Manchester United inapanga kumpa utepe wa unahodha Paul Pogba na pia kuboresha ‘hali’ yake timuni.

Kulingana na jarida la Mirror, Pogba mwenye umri wa miaka 26 tayari ameelekeza macho yake yote ugani Santiago Bernabeu ili kujiunga na Mfaransa mwenzake Zinedine Zidane ambaye aliteuliwa mkufunzi wa Real Madrid mwezi uliopita wa Machi.

Hata hivyo kocha Ole Gunnar Solskajaer anadaiwa kuwa tayari kuandaa mazungumzo kuhusu kumwongezea malipo nyota huyo kupitia kandarasi mpya itakayomweka ugani Old Trafford kwa kipindi kirefu.

Nahodha wa sasa Antonio Valencia tayari amethibitisha kuwa ataagana na Man United mwishoni mwa msimu huu wa 2018/19 huku beki mwenzake Ashley Young akitarajiwa kukabidhiwa majukumu mengine mapya yanayohusu usimamizi wa timu mwishoni mwa msimu.

Pogba ambaye pia ni mshindi wa Kombe la Dunia mwaka wa 2018 na Ufaransa, anatarajiwa kuongoza wenzake kuvaana na Barcelona kwenye kipute cha Klabu Bingwa Barani Uropa (UEFA) Aprili 16, wakilenga kufuta kichapo cha 1-0 na kutinga nusu fainali.