Michezo

Pogba, Lingard waonekana wakizozana

July 9th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA na CECIL ODONGO

NYOTA wa Manchester United Paul Pogba na mshambulizi wa timu hiyo Jesse Lingard, walionekana kwenye farakano Jumanne wakati timu hiyo iliwasili nchini Australia kujifua kwa msimu mpya wa 2019/20.

Kwenye video iliyosambaa katika akaunti ya Twitter ya timu hiyo, Pogba na Lingard walionekana wakikemeana kuhusu suala ambalo bado halijabainika.

Wawili hao walionekana wakitembea wakikaribiana kabla ya Lingard kurusha mikono yake hewani kwa hasira akielekea kwa Pogba.

Raia huyo wa Ufaransa hata hivyo anakasirika na kumkaribia Lingard kisha mlinzi wa Uingereza Victor Lindelof anaingilia kati na kumzingira Pogba

kabla wawili hao kurushiana makonde.

Lindelof pia anaonekana kukerwa na tukio hilo na kuinua mkono wake kumzuia zaidi Pogba kumkaribia mchezaji mwenzake.

Tukio hilo lilifanyika wakati vijana wa kocha Ole Gunnar Solskjaer walikuwa wakitembea na kupunga unyunyu baada ya safari ya saa sita kutoka jiji la Manchester hadi mji wa Perth nchini Australia.

Mashabiki wakerwa

Ingawa hivyo, mashabiki wa Man United wameonyesha kukerwa kwao na tukio hilo huku tetesi za Pogba kuhamia Real Madrid kuungana na kocha Zinedine Zidane ambaye pia ni Mfaransa mwenzake zikizidi kushamiri.

Awali kulikuwa na madai kwamba Pogba alikuwa amesusia ziara hiyo kama njia ya kushinikiza uongozi wa Manchester United kumruhusu ahamie Real Madrid.