Michezo

Pogba na Mourinho warukiana kufuatia sare dhidi ya Wolves

September 24th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

UHASAMA kati ya Kiungo wa Manchester United Paul Pobga na kocha Jose Mourinho unaendelea kutokota baada ya mwanadimba huyo kudai mbinu zisizofaa za ukufunzi wa kocha huyo zilichangia sare waliyosajili dhidi ya Wolverhampton Wanderers Jumamosi Septemba 22.

Baada ya mechi hiyo, Pogba alikashifu  mbinu zilizotumika na Mourinho na kushauri kwamba wangekumbatia mbinu ya kuvamia lango la  wapinzani jinsi walivyofanya dhidi ya majabali Arsenal, Chelsea, Tottenham na Liverpool msimu uliopita wa 2017/2018.

“Tulikuwa nyumbani na tungecheza vizuri zaidi dhidi ya Wolves. Tukiwa nyumbani tunafaa kushambulia hadi dakika za mwisho kwa sababu hapa ni Old Trafford na tuko hapa kushambulia. Nafikiri timu nyingi huogopa Man U kwa sababu ya mpira wa kushambulia ambao hatukuucheza leo na ndilo lilkuwa kosa letu kubwa lililotuponza,” akasema kiungo huyo wa zamani wa Juventus.

Alipoulizwa nani aliwakataza kucheza soka ya kushambulia, mchezaji huyo alijibu kwa kiburi akisema yeye si meneja, kauli ambayo iliashiria alimlenga Mourinho huku akitaka timu itumie mbinu tofauti tofauti za kusakata kabumbu ili kupata ushindi katika mechi zijazo.

“Siwezi kukuambia kwa sababu mimi ni mchezaji tu. Si mimi nafaa kujibu kwasababu mimi si meneja. Siwezi sema zaidi ila  lazima tuwe na mbinu kadhaa za kucheza tukipania ushindi katika mechi zijazo,” akasema Pogba.

Kutokana na uhusiano mbaya kati ya wawili hao, habari zinazomhusisha kiungo huyo na kuguria mabingwa wa Laliga Barcelona zinaendelea kuenea. Sare hiyo ilikuwa pigo kwa Man U ambao sasa wanalemewa na mbio za kupigania ubingwa ingawa msimu huu bado changa.