Habari Mseto

Poghisio amkejeli Lonyangapuo kubadilisha mawaziri kila mara

September 16th, 2019 1 min read

Na OSCAR KAKAI

SENETA wa Kaunti ya Pokot Magharibi, Bw Samuel Poghisio amemsuta Gavana John Lonyangapuo kwa jinsi anavyobadilisha baraza lake la mawaziri mara kwa mara.

Seneta huyo amedai mabadiliko hayo yanaathiri vibaya utekelezaji wa sera za maendeleo.

Haya yanajiri baada ya Prof Lonyangapuo kulifanyia baraza lake la mawaziri marekebisho wiki iliyopita.

Hii ni mara ya pili gavana huyo kufanya mabadiliko kwenye baraza lake tangu achukue ushukani wa kuongoza kaunti hiyo 2017 na kumwondoa naibu wake, Dkt Nicholas Atudonyang kama waziri wa afya.

Prof Lonyangapuo alitetea hatua yake akisema amekuwa akifanya mabadiliko hayo vyema ili kuimarisha huduma katika kaunti hiyo.

Alipuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa mabadiliko hayo yatasaidia mawaziri kufanya bidii na kuinua maisha ya wakazi.

Akiongea na wandishi wa habari mjini Kapenguria, Bw Poghisyo alisema gavana huyo amekuwa akiwabadilisha maafisa wake kila wakati kipindi kipya cha kifedha kinapoanza na hivyo kuathiri utoaji huduma kwa umma.

“Gavana anafaa kushauriana na viongozi wote waliochaguliwa anapofanya maamuzi muhimu ambayo yanagusia utoaji huduma kwa mwananchi,” akasema.