Habari za Kaunti

Pokot Magharibi yamwaga kitita cha Sh600m kupiga jeki elimu

February 27th, 2024 3 min read

NA OSCAR KAKAI

ZAIDI ya wanafunzi 44,000 wamenufaika na fedha za ufadhili wa elimu kwa hisani ya serikali ya Kaunti ya Pokot Magharibi.

Hatua hii ya kuzindua basari ya takriban Sh600 milioni inawaondolea hofu wanafunzi hao ambao masomo yao yangeathirika ikiwa wangetumwa nyumbani kuleta karo.

Kwa muda mrefu, masomo yamekuwa yakiathirika eneo hilo kutokana na changamoto za usambazaji wa fedha za elimu kutoka kwa serikali kuu, usimamizi mbaya wa fedha na baadhi ya wakuu wa shule kukosa uajibikaji na uwazi.

Kila mwanafunzi anayenufaika hupata Sh47,000 ambapo kutoka kwa serikali kuu, serikali ya kaunti na hazina ya fedha za ustawi wa maeneobunge (NG-CDF) viwango huwa ni Sh22,000, Sh20,000 na Sh5,000 mtawalia.

Gavana wa Kaunti ya Pokot Magharibi Simon Kachapin akihutubu Jumatatu kwenye uzinduzi wa basari hiyo katika shule ya kitaifa ya upili ya Chewoyet, alisema kuwa fedha hizo za ufadhili wa elimu ndizo za kiwango cha juu zaidi kote nchini huku akitaka fedha za shule kufanyiwa ukaguzi.

“Fedha za shule zinafaa zikaguliwe. Kulikuwa na masuali kuhusu usimamizi wa fedha za shule ya kitaifa ya Chewoyet lakini mwalimu mkuu anayedaiwa kuhusika na suala hilo hajachukuliwa hatua. Tumegundua kuwa fedha za ufadhili wa elimu kutoka kwa serikali kuu hazitoshi wanafunzi wa shule za mabweni na wengi wanaumia,” alieleza Bw Kachapin, ambaye zamani alikuwa mwalimu mkuu na aliwahi pia kuhudumu kama waziri msaidizi katika Wizara ya Elimu.

Kiongozi huyo alisema kuwa fedha za basari zinalenga kupunguza mzigo ambao familia nyingi hukumbana nao kwa kuelimisha wana wao.

“Tumeongeza basari ya wanafunzi wa shule za mabweni hadi Sh20,000 kutoka kwa Sh15,000 mwaka 2023. Wale ambao wako katika vyuo vya kadri watapata Sh10,000 na wale walioko katika shule za kutwa watapata Sh5,000. Fedha hizi zinaweza kutosha ikiwa zitapata usimamizi bora mwaka mzima,” akasema.

Alisema kuwa fedha hizo zitasaidia wanafunzi kusoma na kupata elimu bora.

“Visa vya ukeketaji, ndoa za mapema na kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia vinachangia viwango vya juu vya ujinga,” alisema.

Bw Kachapin ambaye alitishia kufichua uozo kwenye Wizara ya Elimu ambao hakuweka kidokezo chochote kuuhusu, alisema kuwa baadhi ya shule nchini hupata mgao mkubwa kuliko nyingine.

“Baadhi ya shule hupata mamilioni ya pesa kuliko shule nyinginezo. Wabunge wetu huogopa kuongelea suala hilo bungeni… kazi yao ni kupiga siasa kila wakati,” alisema Bw Kachapin.

Bw Kachapin alisema kuwa mwaka wa kifedha wa 2022/2023 walipeana basari ya Sh435 milioni ambazo zilinufaisha wanafunzi 41,413.

Alisema kuwa walionufaika ni wanafunzi 22,000 wako katika shule za mabweni huku 12,000 wakiwa katika shule za kutwa nao 6,000 wakiwa katika vyuo vya kiufundi, vyuo vya mafunzo ya walimu, na vyuo vya utabibu, nao 3,686 wakiwa katika vyuo vikuu.

Alisema kuwa basari za kaunti zinasaidia fedha za serikali kuu ambazo usambazaji wake uko na changamoto kufika shuleni.

“Ikiwa walituma Sh9,000 pekee mwaka 2023 basi kuna shida. Ikiwa serikali kuu haitumi fedha hizo shuleni, basi tuko na shida,” alisema gavana huyo.

Alisema kuwa kaunti hiyo imetenga Sh20 milioni za kuboresha miundomsingi katika shule 40 ambapo 22 ni za msingi huku 18 zikiwa ni za upili. Lengo la uboreshaji huo alisema ni kubuni mazingira bora ya wanafunzi.

“Tuko na mipango ya kuinua vyuo vya anuwai na tayari wakufunzi 14 wameajiriwa kwenye vyuo saba katika kaunti,” alisema Bw Kachapin.

Kamishina wa Kaunti ya Pokot Magharibi Khalif Abdulahi aliwaonya walimu wakuu kuhusu kuitisha viwango vya karo juu kupitiliza kiwango kilichokubalika na pia kuwatuma wanafunzi nyumbani kuleta karo.

“Wanafunzi wanafaa kusalia shuleni. Ni makosa makubwa kutuma wanafunzi nyumbani. Hii sio sera ya Wizara ya Elimu. Tunataka kuonya walimu wakuu dhidi ya kulazimisha wanafunzi kulipa karo zisizofaa kama fedha za kuwapa morali walimu, masomo ya ziada na kununua karatasi… Hii ni kwa sababu serikali inalipa karo ya shule za upili,” alisema Bw Abdulahi.

Alisema kuwa watahakikisha kuwa wanafunzi asilimia 100 kutoka shule za msingi wanajiunga na zile za upili.

Kamishina huyo aliagiza manaibu kamishina, makamishina wa tarafa, machifu na manaibu wao kuhakikisha watoto wote katika eneo hilo wako shuleni

“Kupandishwa ngazi kutategemea idadi ya wanafunzi ambao wameenda shule kutoka eneo lako,” akasema

[email protected]