Michezo

Polack alenga kukisuka upya kikosi cha Gor Mahia

May 28th, 2020 1 min read

Na CECIL ODONGO

GOR Mahia imeanza mikakati ya kujitayarisha kwa msimu ujao huku kocha Steven Polack akitarajiwa kukisuka upya kikosi chake ili kuiwezesha timu hiyo kutamba kwenye mashindano ya Bara Afrika.

Polack alisema kwamba ana habari huenda wachezaji wake tegemeo wataondoka kutafuta ujira kwingine, ndiyo maana ameanza kujipanga mapema kwa ajili ya msimu ujao.

“Kwa kuwa hatima ya Ligi Kuu (KPL) sasa ipo mbele ya mamlaka husika, ni vyema ifahamike kwamba nimeanza kuelekeza macho yangu kwenye msimu unaokuja. Hii inahusisha kuwatambua wachezaji wa kuwasajili kuziba pengo la wale watakaondoka. Pia wachezaji wa sasa wanaendelea na mwongozo wa kufanya mazoezi hadi tujue hatima ya msimu huu,” akasema Polack kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Gor ambayo imekuwa ikabiliwa na matatizo chungu nzima ya kifedha, huenda ikawapoteza wachezaji wake mahiri msimu ujao iwapo hawatapata mdhamini mpya.

Ukosefu wa ngwenje umekuwa ukikabili timu hiyo tangu kujiondoa kwa waliokuwa wadhamini wao Sportpesa.

Wachezaji wa K’Ogalo, mnyakaji David Mapigano, winga Dickson Ambudo wote kutoka Tanzania na Juma Balinya kutoka Uganda tayari wametishia kwamba watakatiza huduma zao na K’Ogalo iwapo hawatalipwa malimbikizo ya mishahara yao.

Pia kumekuwa na madai kwamba wachezaji kutoka hapa nchini ambao hawajaridhishwa na uchechefu wa kifedha ndani ya K’Ogalo wapo guu moja nje ya mabingwa hao mara 18 wa KPL.

Ingawa hivyo, Polack anasisitiza kwamba anatathmni wachezaji wakali wa kusajiliwa na uongozi wa timu hiyo ili kuwavumisha msimu ujao.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba huenda akawatoa wachezaji wengine kutoka kwa kikosi cha vijana cha K’Ogalo na kuwapandisha hadi kikosi cha kwanza.

Washambulizi Kennedy Agogo na Lloyd Khavuchi ni kati ya wanasoka ambao walipandishwa ngazi kutoka kikosi kichanga cha Gor hadi timu ya kwanza msimu huu.