Michezo

Polack asema wachezaji hawafai kumlaumu kwa kukosa posho

May 24th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

MKUFUNZI wa Gor Mahia Steven Polack amesema wachezaji wa timu hiyo hawafai kumlaumu kwa kutowapigania walipwe malimbikizo ya mishahara yao wakati huu wa janga la virusi vya corona.

Polack amesikitishwa na ripoti kwamba wanasoka wake wanamalumu kwa kukimya huku wakiendelea kuteseka kwa kutolipwa fedha zao kwa miezi kadhaa.

Aidha ripoti hizo zilidai wachezaji hao wamekuwa wakipigania walipwe fedha zao kivyao huku kocha huyo akionekana kutoshughulishwa na suala hilo.

Hata hivyo, Polack amejitetea akisema kwamba amekuwa akiusukuma uongozi wa Gor uwalipe wachezaji wake mishahara, akifichua kwamba hata yeye pia hajalipwa fedha zake.

Kocha huyo raia wa Uingereza aliwashutumu baadhi ya watu wasiofurahia uwepo wake klabuni humo kama wanaochochea wachezaji dhidi yake ilhali yeye huwa halipi mishahara.

Aidha alitishia kuwafichua watu ambao wamekuwa wakiwahangaisha wachezaji hao wanapojaribu kufikia uongozi wa klabu kudai hela zao.

“Wale ambao wanasema sina nia ya kuwasaidia wachezaji kupokea fedha zao ni waongo na wanafiki. Nimekuwa nikishinikiza uongozi wa Gor kuwalipa wachezaji na kila mara niko kwa afisi ya mwenyekiti wetu kuulizia hatua zilizopigwa kuhusu suala hilo. Najua nyakati ni ngumu bila fedha lakini tuvumiliane na kutia subira,” akasema Polack.

Ingawa wachezaji wa Gor hawajalipwa mishahara kwa miezi kadhaa, uongozi wa klabu mara kwa mara umekuwa ukiwapa vijipeni vichache kuwasaidia kujikimu na pia kulipia kodi.

Hali ni hiyo hiyo kwa watani wao wa jadi AFC Leopards ambao pia wanasoka wake wanakabiliwa na njaa tangu kutoweka kwa wadhamini wao SportPesa mnamo Agosti 2019.

“Watu wanaishi kwa nyakati ngumu na naelewa wachezaji wangu pia wanaumia kwa kukosa kodi na vyakula. Kimya changu hakimaanishi kwamba siwapiganii wanasoka wangu; fedha ndizo hakuna kwa sasa,” akaeleza Taifa Leo.

Kauli ya Polack inajiri huku ikiripotiwa baadhi ya wanasoka tegemeo wa K’Ogalo wameamua kuguria timu nyingine msimu ujao kwa kukosa kulipwa fedha zao.

Gor wanaongoza msimamo wa jedwali kwa alama 54 ligi ikiwa imesitishwa kutokana na janga la corona, zikiwa zimesalia mechi 10 msimu ukamilike.