Poland na Uhispania nguvu sawa kwenye Euro

Poland na Uhispania nguvu sawa kwenye Euro

Na MASHIRIKA

FOWADI na nahodha Robert Lewandowski alifunga bao lake la kwanza kwenye fainali zinazoendelea za Euro na kusaidia timu ya taifa ya Poland kuwalazimishia Uhispania sare ya 1-1 ambayo iliweka hai matumaini yao ya kufuzu kwa hatua ya 16-bora.

Poland walijibwaga ugani wakijua kwamba wangekosa kusonga mbele kutoka Kundi E iwapo wangezidiwa maarifa na Uhispania waliowekwa kifua mbele na Alvaro Morata katika dakika ya 25.

Baada ya kushindwa kutambisha Poland katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi E ulioshuhudia Slovakia wakisajili ushindi wa 2-1 mnamo Juni 14, Lewandowski anayechezea Bayern Munich alijituma vilivyo na akasawazisha dhidi ya Uhispania katika dakika ya 54.

Uhispania walipata fursa nzuri ya kufunga bao la ushindi katika kipindi cha pili baada ya refa Daniele Orsato kuwapa penalti kutokana na tukio la Gerard Moreno kukabiliwa visivyo ndani ya kijisanduku cha Poland. Hata hivyo, Moreno alishuhudia kombora lake likigonga mhimili wa goli la Poland huku jaribio la Morata la kurejesha mpira huo langoni zikiambulia patupu.

Mchezaji mwingine wa Uhispania ambaye alipoteza nafasi za wazi za kufungia Uhispania bao la ushindi ni fowadi wa Manchester City, Ferran Torres ambaye kwa pamoja na Morata, walimwajibisha sana kipa Wojciech Szczesny wa Poland mwishoni mwa kipindi cha pili.

Sare dhidi ya Poland inamaanisha kwamba Uhispania ambao ni mabingwa mara tatu wa Euro bado hawana ushindi wowote kwenye fainali za kipute hicho mwaka huu. Uhispania waliambulia sare tasa dhidi ya Uswidi katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi E mnamo Juni 14, 2021.

Mabingwa hao wa dunia mnamo 2010, sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye Kundi E kwa alama mbili. Slovakia wanakamata nafasi ya pili kwa pointi tatu huku Uswidi wakidhibiti kilele kwa alama nne. Chini ya kocha Luis Enrique, Uhispania watacheza na Slovakia katika mchuano wa mwisho wa Kundi E mnamo Juni 23 huku Poland wakivaana na Uswidi siku hiyo.

Uhispania hawajawahi kushinda mechi mbili za ufunguzi kwenye kampeni za Euro tangu 1996. Kati ya 2008 na 2012, Uhispania walikuwa tishio kubwa kwa vikosi vingine vya soka duniani huku wakishinda Kombe la Dunia na mataji mawili ya Euro katika kipindi hicho cha muda.

Miamba hao walifahamika pakubwa kwa mtindo wao wa ‘tiki-taka’ ambao ni kucheza kwa kasi na kupokezana pasi fupifupi za haraka zenye uhakika. Japo walitamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira katika mechi iliyowashuhudia wakikamilisha pasi 954 dhidi ya Uswidi, Uhispania waliokota alama moja pekee baada ya sare tasa.

Walicheza kwa mtindo uo huo wa kutabirika dhidi ya Poland ila wakakosa makali ya kufunga mabao kwenye safu yao ya mbele.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ufaransa wakabwa koo na Hungary katika mchuano wa Euro

Wanaume wahimizwa kuwajibikia vilivyo majukumu yao katika...