Poleni mashabiki, yalikuwa tu majaribu ya kimwili – Samidoh

Poleni mashabiki, yalikuwa tu majaribu ya kimwili – Samidoh

Na SAMMY WAWERU

MASHABIKI wangu ninawaomba msamaha kwa kuteleza, kuwa na mpango wa kando ulioishia kujaaliwa mtoto ambaye hana hatia, amesema mwanamuziki tajika wa nyimbo za benga kwa lugha ya Agikuyu, Bw Samuel Muchoki.

Akikiri kuwa kwenye uhusiano haramu na mwanasiasa mmoja jijini Nairobi, staa huyo maarufu kama Samidoh, Jumanne kupitia mitandao ya kijamii aliomba mashabiki wake msamaha kwa kile alitaja kama “kuweka mfano mbaya katika jamii”.

Uhusiano wa msanii huyo anayefahamika kwa nyimbo zinazoongoa mashabiki wake katika jamii ya Kikuyu kama vile Ndiri Mutwe (sina kichwa/akili timamu), Kairitu Gakwa (binti yangu), Wendo Wi Cama (upendo wenye raha na tamu), kati ya vibao vinginevyo, na mwanasiasa Karen Nyamu, umekuwa gumzo mitandaoni wengi wakimkashifu na kumsuta vikali kwa jaribio kuvunja ndoa yake.

Bi Karen na ambaye katika uchaguzi mkuu wa 2017 aliwania kiti cha mwakilishi wa wanawake Nairobi, siku kadha zilizopita alipakia kwenye akaunti zake za mitandao video ya Samidoh akimpakata na kucheza na mwanawe wa pili.

“Baba hakuelezi kwamba anakupenda, anathibitisha kwa matendo #Muchokis,” maandiko ya Karen yakaandamana na chapisho hilo.

Karen pia amesisitiza kwamba hatasita kupakia picha na video za familia yake, wakati anaotaka.

Akiomba radhi mashabiki wake wanaomfuatilia mitandaoni, Samidoh amethibitisha kwamba yeye ndiye baba wa mtoto huyo wa kiume.

“Poleni! Nimeiweka familia yangu na mimi mwenyewe katika hali mbaya. Ni kweli nilikuwa na uhusiano na Bi Karen Nyamu, na ni kupitia urafiki huo mtoto asiye na hatia alizaliwa.

“Nitaendelea kusaidia mwanangu kwa hali na mali. Mimi ni baba anayejivunia na kupenda watoto wake,” Samidoh akaelezea kwenye chapisho la Facebook.

Muimbaji huyo akionekana kumkosoa wakili Karen, ameeleza kusikitishwa na nia ya video inayosambaa mitandaoni, anayoonekana akipakata mwanawe.

“Ninasumbuliwa na nia ya video hiyo ambayo imesababisha mtoto (akimaanisha aliyepata na Karen) na mke wangu kushambuliwa mitandaoni. Sijawahi kumuacha mke wangu ambaye nimeishi naye miaka 11 mfululizo kwa sababu ya mwanamke mwingine,” msanii huyo akasema.

Aidha, Bw Samidoh amedokeza kwamba ameomba radhi mke wake ambaye wapekuzi mitandaoni wamemtambua kama Edday Nderitu na pia familia yake.

“Niliomba mke wangu na familia yangu msamaha. Kwa sasa ninawaomba radhi mashabiki wangu kwa kuweka mfano mbaya. Ninakiri na kukubali makosa yangu, ninayajutia. Tumekuwa tukipitia milima na mabonde, ila tunasalia imara na wenye furaha pamoja,” akafafanua Bw Samidoh ambaye pia ni afisa wa polisi.

Baadhi ya wachangiaji mitandaoni wameridhia hatua ya dharura aliyochukua.

“Ndugu yangu mdogo, Samidoh hii ni hatua nzuri. Sasa, yule mwanadada mwingine aheshimu mke wako na awache madharau. Akuheshimu na aheshimu familia yako…Nimekuwa nikisubiri hili ndugu yangu…” akachangia Sammy Ondimu Ngare, afisa wa polisi na pia mwanamuziki.

“Tunahitaji wanaume kama wewe hii Kenya. Ndio maana ninaridhishwa nawe, ukomavu wako ni wa hali ya juu. Kosa ni kosa tu, chunga familia na watoto wako. Baraka Samidoh.” #Wambui Wa Waithira akaelezea.

“Nimefurahishwa na hatua uliyochukua. Unyenyekevu wako uko kwenye daraja lingine. Asante kwa kukubali makosa, hakuna aliye kamilifu. Mungu aibariki ndoa yako,” akasema Purity Ng’ethe.

You can share this post!

Mwanasiasa yeyote asijiapishe tena kama Raila, ni haramu...

Mhasibu akana kutafuna Sh22 milioni