Habari za Kitaifa

Polisi 4 wanaodaiwa kuiba pombe yenye sumu na kuuzia mfanyabiashara wazuiliwa

February 13th, 2024 2 min read

NA GEORGE MUNENE

MAHAKAMA ya Baricho mnamo Jumanne iliwaruhusu polisi kuwazuilia wenzao wanne wanaodaiwa kuiba pombe vyenye sumu inayoaminika kuwaua watu 15 katika kijiji cha Kangai, Kaunti ya Kirinyaga kwa siku 15 ili kuwezesha wapelelezi kukamilisha uchunguzi wao.

Pombe hiyo ilikuwa eksibiti kabla ya kudaiwa kuibwa na maafisa hao na kuuzia mfanyabiashara wa eneo hilo, John Muriithi Karaya, ambaye pia alifikishwa kortini jana. Maafisa hao akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) cha Kiamaciri walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Stephen Munene Nyaga asubuhi lakini hawakuhitajika kujibu mashtaka.

Maafisa hao Francis Mutethia, Brian Kariuki, Allan Kimanzi na Kenneth Mugambi (OCS) walinaswa Jumatatu na kuzuiliwa katika kituo cha polisi ya Kiamaciri.

Afisa wa uchunguzi wa Jinai, Michael Cheruiyot alifahamisha mahakama kuwa muda zaidi ulihitajika ili kufanya uchunguzi wa kina.

Alisema eksibiti ambazo ni pamoja na ethanol ambayo ilikuwa na kesi mahakamani na ambayo iliibwa katika kituo cha polisi cha eneo hilo inashukiwa kusababisha vifo vya watu 15.

Alisema uchunguzi wa miili ya marehemu haujafanyika na eksibiti zinatakiwa kupelekwa kwa maabara ya Serikali kufanyiwa uchunguzi.

Bw Cheruiyot alisema maafisa hao ambao wanashtakiwa pamoja na raia mmoja kwa jina Anthony Muthee, huenda wakaingilia uchunguzi iwapo wataachiliwa.

Maafisa hao watazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kerugoya hadi Machi 7 kesi hiyo itakapotajwa.

Inadaiwa walivamia stoo katika kituo cha polisi cha Kiamaciri katika Kaunti Ndogo ya Mwea Magharibi na kuiba vielelezo ambavyo wanadaiwa kumuuzia mfanyabiashara wa eneo hilo.

Uchunguzi utakapokamilika, maafisa hao watashtakiwa kwa wizi, kula njama ya kutenda uhalifu na kuzuia haki kutendeka.

Awali, maafisa hao walilalamika kuwa walidhulumiwa wakiwa katika seli na wakaomba mahakama kuingilia kati.

Bw Karaya alikanusha shtaka la kupatikana akiuza pombe iliyoisha muda wake wa kutumika katika soko la Kandongu, kaunti ndogo ya Mwea Magharibi mnamo Februari 7.

Alilalamika kuwa polisi wamekuwa wakilenga baa yake na akadai anahofia usalama wake katika kituo cha polisi cha Kiamaciri.

Mahakama ilikubali ombi la upande wa mashtaka asiachiliwe kwa dhamana kwa kuwa uchunguzi unaendelea na ikaagiza azuiliwe katika kituo cha polisi cha Sagana hadi Machi 7.