Makala

Polisi adaiwa kumjeruhi dereva ndani ya seli kwa bifu ya hongo

March 29th, 2024 3 min read

NA OSCAR KAKAI

POLISI mmoja anatuhumiwa kumpiga na kumjeruhi vibaya dereva wa matatu inayohudumu kwenye barabara ya Kitale-Kapenguria akiwa ndani ya seli katika kituo cha polisi cha Kapenguria, Kaunti ya Pokot Magharibi.

Inadaiwa afisa huyo alimuumiza dereva huyo katika sehemu nyeti mnamo Machi 20, 2024.

Inadaiwa pia alikuwa amekerwa kwa kunyimwa hongo siku za awali katika kizuizi cha polisi barabarani.

Siku ya tukio, Bw Nelson Mwasame, 38, ambaye ni baba wa watoto wane, aliamka mapema kama kawaida na kutoka nyumbani kwake eneo la Kipsaina, Kaunti ya Trans Nzoia na kuelekea kazini ndani ya gari la kazi

Akiwa kwenye barabara, abiria wa kawaida waliingia kwa gari hilo akiwemo mwanamke ambaye alipandia steji ya pili almaarufu B kwenye kituo cha magari cha Kesogon.

Kulingana na Bw Mwasame, hakusikia ombi la abiria huyo ambaye alitaka kushukia eneo la Makutano ya Talau.

“Sikusikia abiria akiniambia nisimamishe gari kwa sababu sauti ya redio ilikuwa juu. Alikuwa ameketi nyuma kabisa ndani ya gari,” akaeleza Bw Mwasame.

Bw Mwasame anaeleza kuwa gari hilo lilipita kilomita kadhaa na mwanadada huyo mwenye ghadhabu akashukia katika makutano ya Tartar Weighbridge.

“Alishuka na kunitusi kuwa mimi ni mjinga na kwamba angenifunza adabu,” anasema.

Dereva huyo anasema kuwa abiria huyo alikataa kulipa nauli ya kawaida ya Sh70 na badala yake akalipa Sh50 pekee.

Tofauti zao, imadaiwa ziliishia wao kurushiana matusi, suala ambalo lilifanya mwanamke huyo kupiga ripoti katika kituo cha polisi.

Kufika mjini Kapenguria, Bw Mwasame alishikwa na polisi kwa kumtusi abiria mwanamke. Alipelekwa katika kituo cha polisi cha Makutano.

“Nilifika mjini Kapenguria majira ya saa kumi na mbili na nusu na nikashikwa. Nilitaka niachiliwe kwa bondi ya polisi lakini nikanyimwa. Saa nne usiku nilihamishwa hadi kituo cha polisi cha Kapenguria,” anasema.

Akiwa kwenye kituo cha polisi cha Kapenguria, Alhamisi usiku, Bw Mwasame anasemekana kupigwa na kujehuriwa na afisa aliyekuwa kwa zamu.

Mwathiriwa alijeruhiwa vibaya na sasa suala hilo limezua mdahalo mkubwa miongoni mwa wakazi.

Suala la maadili ya polisi linaangaziwa.

“Tulikuwa watu saba ambao tulikuwa tumeletwa kwenye seli lakini jina langu halikuitwa kuingia ndani. Wengine waliingizwa na nikabaki sehemu ya kuandikishwa. Afisa mmoja wa polisi ambaye alitupiga sachi hakuniongelesha,” anasema.

Anasema afisa huyo baadaye alianza kumhoji, kumdhalilisha kisha akampiga kofi.

“Alinisukuma ndani ya seli. Baada ya dakika 15, afisa huyo wa polisi alikuja akiwa ameshika pombe, tochi na rungu mkononi,” anadai.

Bw Mwasame ambaye anaeleza masaibu yake akiwa katika wadi ya kwanza katika hospitali ya rufaa ya Kapenguria, anasema kuwa afisa huyo alimpeleka kwenye chumba kingine chenye giza na kuanza kumuuliza sababu ya yeye kushikwa.

“Lakini pia aliniuliza sababu ya mimi kumnyima pesa kila siku. Alidai mimi huwa ninapeana hongo kwa afisa wa trafiki na si yeye. Alinipiga vibaya na rungu,” anasema.

Dereva Nelson Mwasame, 38, akiwa hospitalini Kapenguria. PICHA | OSCAR KAKAI

Bw Mwasame anasema kuwa afisa huyo ni mtu ambaye anamfahamu vizuri sababu yeye humuona kwenye kizuizi cha polisi barabarani.

“Alinipiga vibaya akiniuliza sababu ya mimi kupea hongo afisa wa trafiki na sio yeye. Alidai kuwa mimi huwaona kama watu feki. Aliniambia nitoe nguo aone kama nimetahiriwa. Alivuta sehemu zangu za siri na kunichuna.  Alinilazimisha kunywa pombe lakini nikamwambia kuwa sinywi pombe. Alimwaga maji sakafuni na kunilazimisha nilale pahala baridi. Nililia kwa uchungu nikitaka msaada. Nilizirai kisha akaleta maji kwa ndoo na kunifanyia huduma ya kwanza,” anasema.

Mwathiriwa huyo alipelekwa katika hospitali ya rufaa ya Kapenguria na maafisa wa polisi wa kituo hicho baada ya kupewa bondi.

Anadai kuwa afisa huyo ako na uchungu na yeye sababu ya kukosa kumpa hongo kwenye kizuizi cha polisi barabarani.

Bw Mwasame sasa anataka haki kutendeka.

“Mimi sikuwa mlemavu lakini mwanadamu amenilemaza. Ninataka haki na serikali inisaidie. Mguu wangu umekufa ganzi na nina majeraha katika sehemu zangu za siri na kiuno,” anasema.

Mkewe Bw Mwasame, Bi Rose Nelson, anasema kuwa mumewe ni tegemeo la familia na sasa huenda hatafanya kazi kama kawaida.

“Ninasikia uchungu.Tuko na watoto wanne na wawili wako katika shule ya upili. Mimi sina kazi na mume wangu ndiye tegemeo langu na sasa amekuwa mlemavu,” akasema Bi Nelson.

Anatoa wito kwa Mamlaka ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (Ipoa) kuingilia kati suala hilo.

Bw Joseph Mwasame, nduguye mwathiriwa, anasema kuwa suala hilo ni dhuluma kwa Wakenya wasiokuwa na hatia.

“Hawezi kutembea. Tunambeba kama mtoto tukimpeleka haja ndogo na kujisaidia kwingine,” anasema Joseph.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Pokot Magharibi Kipkemoi Kirui alithibitisha kuwa kesi hiyo iliripotiwa Machi 20, 2024.

Bw Kirui anasema mwanamume huyo ambaye alikuwa kwenye seli, aliumizwa na afisa wa polisi kwa jina Joseph Kamau.

Anasema kuwa uchunguzi unaendelea lakini wamechukua hatua na mwathiriwa yuko hospitalini.

“Tunataka mwathiriwa kupona na akuje kuandikisha taarifa. Mahabusu wengi walishuhudia shambulio hilo,” anasema Bw Kirui.

Alisema kuwa hatua hali zitachukuliwa dhidi yake ikiwa atapatikana na makossa

“Afisa huyo anafanya kazi lakini tutamchukulia hatua kali. Ikiwa atapatikana na makosa tutampeleka mahakamani. Yeye hayuko juu ya sheria. Atakuwa kama mfano kwa wengine. Sisi hatujasikia kuhusu madai ya ufisadi lakini wawili hao wanajuana,” akasema Bw Kirui.

[email protected]