Habari

Polisi afyatua risasi hewani mtihani ukiendelea

October 31st, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MTIHANI wa Darasa la Nane (KCPE) unafikia tamati leo Alhamisi huku visa vingi vikushuhudiwa jana Jumatano katika sehemu mbalimbali nchini.

Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, kulikuwa na wasiwasi katika Shule ya Msingi ya Malazi ya Kiini katika Kaunti Ndogo ya Maara, baada ya polisi aliyekuwa akilinda mtihani huo kufyatua risasi hewani kimakosa.

Tukio hilo liliwafanya wanafunzi na wasimamizi wa mtihani huo kukimbilia usalama wao.

Kulingana na ripoti za polisi, kisa hicho kilifanyika mwendo wa saa saba u nusu alasiri, baada ya wanafunzi kumaliza kufanya Mtihani wa Kiingereza. Polisi huyo, aliyetambuliwa kama Harrison Mutheke alifanya kitendo hicho kwa kutumia bunduki yake aina ya G3 lakini hakuna aliyejeruhiwa. Msimamizi wa mtihani huo katika shule hiyo Bi Mary Muthoni aliripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Mitheru.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Maara Bw Johnston Kabusia alizuru katika shule hiyo ambapo aliagiza mshukiwa kukamatwa na kunyang’anywa bunduki hiyo. Inadaiwa polisi huyo alikuwa mlevi.

Katika kaunti iyo hiyo, watahiniwa 11 walioacha masomo yao mwaka huu baada ya kujiunga na Kanisa la Kavonokia hawakujitokeza kufanya mtihani wao katika Kaunti Ndogo ya Tharaka Kaskazini. Watahiniwa hao pia hawakupatikana nyumbani mwao baada ya kutafutwa.

Katika Kaunti ya Nyamira, mtahiniwa mmoja alifariki katika Shule ya Msingi ya Gwetebe, baada ya kuchomwa na stima wakati wenzake walikuwa wakila chakula cha mchana. Kisa hicho kilithibitishwa na Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Bw Amos Mariba.Katika Kaunti ya Nyandarua, polisi waliwakamata watu wanane katika Shule ya Msingi ya Kibinafsi ya Hezta kwa tuhuma za kuendesha njama za kufanya udanganyifu katika mtihani huo.

Katika Kaunti ya Nairobi, Naibu Rais William Ruto alikuwa miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali walioshuhudiwa uendeshaji wa mtihani huo. Dkt Ruto alifika katika Shule ya Msingi ya Ngong Forest, ambapo wanafunzi walikuwa wakianza kuufanya Mtihani wa Sayansi. Dkt Ruto aliwahakikishia Wakenya kwamba serikali imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha kuwa watahiniwa wanaufanya mtihani huo bila matatizo yoyote.

Katika Kaunti ya Kakamega, watu wanane wakiwemo wasimamizi kadha wa mtihani huo katika Kaunti Ndogo ya Matungu wanachunguzwa na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa tuhuma za kukiuka kanuni za uendeshaji wake.

Wanane hao wanajumuisha mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Ngairwe, msimamizi mkuu Bw Washington Magero na wasimamizi wengine sita.

Wasimamizi hao wanazuiliwa baada ya kupatikana na simu zao shuleni humo. Vile vile, waliruhusu walimu watatu ambao wamo likizoni kurejea katika hali tatanishi.

Kulingana na kanuni za KNEC, ni makosa kwa wanafunzi, wasimamizi wa mitihani ama walimu wakuu kupatikana na simu za rununu katika vituo vya kufanyia mitihani. Walimu hao waliotambuliwa kama Mabwana Edwin Keya, Ferdinard Balungu na Bi Scholastica Osodo walikamatwa baada ya kujifanya kuwa wapishi wa shule hiyo.

Katika Kaunti ya Makueni, Waziri wa Elimu Prof George Magoha alieleza kuridhishwa na kupungua kwa idadi ya watahiniwa waliojifungua watoto kwenye mtihani wa mwaka 2019.

 

Na Pius Maundu Alex Njeru, Faith Nyamai, na Shaban Makokha