Polisi ahepa kazi Mombasa kufukuzia penzi la mama waliyekutana mtandaoni

Polisi ahepa kazi Mombasa kufukuzia penzi la mama waliyekutana mtandaoni

Na MWANGI MUIRURI

POLISI mjini Maragua katika Kaunti ya Murang’a wanachunguza kisa ambapo afisa wa polisi anadaiwa alisafiri kutoka Mombasa hadi mji huo mdogo kuishi na mwanamke aliyempa mwaliko kupitia mtandao.

Polisi walisema afisa huyo, ambaye anahudumu katika kikosi cha RDU jijini Mombasa, alisafiri Machi 27 hadi Maragua alikopokelewa na mwanamke waliyekutana kupitia mtandao wa kijamii.

Kamishna wa Murang’a, Mohammed Barre alisema afisa huyo alikamatwa Alhamisi jioni kusaidia katika uchunguzi kuhusu alivyohepa kazi.

“Polisi wanachunguza kilichomfanya afisa huyo kuhepa kazi bila uhamisho rasmi. Pia wanachunguza kama ni ukweli kwamba akiwa mjini Maragua amekuwa akihangaisha watu usiku akijifanya afisa wa polisi,” akasema.

Mwanamke aliyemwalika mwanamume huyo anaripotiwa kuwa na umri wa miaka 41 na mama wa vijana watatu wa kiume wa kati ya miaka 16 na 23.

Wakazi wa Maragua walisema baada ya afisa huyo kufika mjini humo, alikaa nyumbani kwa mwanamke huyo kwa muda mfupi kisha akafukuzwa.

‘Baadaye alihamia katika kontena inayomilikiwa na mwanamke huyo, na kwa siku nne mfululizo alikuwa akilala sakafuni bila hata cha kujifunika. Hakuwa na hata ndururu mfukoni mwake,’ akasema mmoja wa majirani wa mwanamke huyo.

Wakazi baadaye walipiga ripoti polisi kuhusu mwanamume huyo wakishuku hakuwa na nia njema.Kumekuwa na ongezeko la visa vya wanaume na wanawake ambao wanakutana kwenye mitandao, ambapo baadhi wameishia kujuta baada ya kuhadaiwa.

Kuna wengine ambao wamedhulumiwa na hata kuuawa na watu ambao wamekutana nao kupitia mitandao ya kijamii.

You can share this post!

Wanahabari wa spoti wa NMG watwaa tuzo

Wandayi akana muungano kati ya Raila na Ruto