Habari za Kaunti

Polisi ajiumiza mwenyewe kwa risasi mdomoni

January 3rd, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

POLISI wa kiume anayehudumu katika Kaunti ya Murang’a, amekimbizwa hospitalini akiwa hali mahututi baada ya kudaiwa kujipiga risasi mdomoni akilalama kuwezwa na maisha ya ulevi.

Kwa mujibu wa ripoti ya dharura ambayo imeandaliwa na kamati ya kiusalama ya Murang’a na kituo cha polisi cha Kangema, ni kwamba “kwa sasa afisa huyo amekimbizwa katika hospitali ya Murang’a Level 5”.

Imeelezewa kwamba afisa huyo aliyeonekana kutatizika kimawazo kuanzia nyakati za asubuhi alikuwa amepewa ruhusa ya kupumzika lakini jioni, kukasikika mlio wa risasi iliyofyatuliwa kwa bunduki kwake.

“Wakati maafisa wengine walifika kujua kulikoni, walimpata akiwa amelala hoi huku bunduki yake ndogo bado ikiwa bado mdomoni na damu ikimtiririka,” ripoti hiyo yasema.

Kamanda wa polisi wa Murang’a Bw Mathiu Kainga alisema kwamba kisa hicho kinachunguzwa.

“Kwa sasa hatuwezi tukamtambulisha afisa huyo kwa umma kabla ya kujadiliana na familia yake,” akasema Bw Kainga.

Aidha, alisema kwamba “hatujapata ripoti ya kina kutoka kwa madaktari wanaomshughulikia”.

Msimamizi mkuu wa hospitali ya Murang’a Dkt Leonald Gikera alisema kwamba “kwa sasa juhudi za kupiga msasa ripoti za picha kufahamu kiwango cha jeraha na kama risasi imekwama ndani ya mkondo wa ilipopenyea unaendelea na ripoti kamili itaandaliwa”.

Hali ya afisa huyo ilielezewa kuwa “dharura lakini inayoshughulikiwa kwa mujibu wa mikakati ya kiutaalam”.