Habari Mseto

Polisi akamatwa baada ya kuua mtu akidai ni jambazi

March 31st, 2019 1 min read

Na Lucy Mkanyika

Polisi mjini Taveta, Kaunti ya Taita Taveta, wamemtia mbaroni mwenzao kwa kumuua mwanamume mmoja Ijumaa usiku. Kisa hicho kilitokea katika baa ya Rockland mjini humo.

Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, afisa huyo alimpiga risasi mwanamume huyo akidai alikuwa jambazi.

Walidai kuwa afisa huyo aliyetambulia kama David Gitahi alikuwa mlevi wakati alipotekeleza kisa hicho.

Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi wa eneo hilo Bw Lawrence Maroa alisema kuwa afisa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Taveta kwa kumuua Bw Esau Juma.

Bw Maroa alisema Bw Gitahi alikuwa amekabidhiwa bunduki ili kupiga doria usiku huo.

Alisema kuwa mwendazake alikuwa akiburudika na wenzake kabla ya kupigwa risasi.

“Tumeanzisha uchunguzi kuhusu kisa hiki tujue kile hasa kichojiri,”alisema.

Bw Maroa alisema kuwa afisa huyo alidai marehemu alikuwa miongoni mwa majambazi sugu wanaotafutwa kwa kuua mpelelezi wa DCI wiki jana katika eneo hilo.

“Tulipomkamata tuligundua kuwa alikuwa mlevi. Alituambia kuwa hakuwa na makosa kwani mwendazake ni mwizi tunayemsaka,”alisema. Alisema kuwa walipata maganda matatu ya risasi eneo la mkasa.

Mwili wa Bw Juma unahifadhiwa katika hospitali ya Taveta ukingojea kufanyiwa upasuaji.