Polisi akana kumuua mwenzake kituoni

Polisi akana kumuua mwenzake kituoni

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi aliyempiga risasi 10 rafikiye ndani ya kituo cha polisi baada ya kutafuna miraa Jumatano alishtakiwa kwa mauaji.

Konstebo Edgar Mokamba alikanusha shtaka la kumuua Zachary Makuto Simwa mnamo Desemba 30 mwaka uliopita katika kituo cha polisi cha Nyali kaunti ndogo ya Westlands Nairobi.

Alisomewa shtaka kwa njia ya mtandao akiwa katika kituo cha polisi cha Gigiri kisha akapelekwa kuzuiliwa gereza la Viwandani Nairobi.

APC Mokamba alikana shtaka la kuua akikusudia mbele ya Jaji Daniel Ogembo wa Mahakama kuu ya Milimani Nairobi.

Mshtakiwa huyo anayetetewa na wakili Danstan Omari aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “ hatatoroka akipewa dhamana na kwamba atahudhuria vikao vyote vya kusikizwa kwa kesi inayomkabili.

“Naomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana, yeye ni afisa wa polisi na anaelewa barabara athari za kutofika kortini,” Bw Omari alimweleza Jaji Ogembo.

“Je uko na maagizo upinge mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana,” Jaji Ogembo alimwuliza kiongozi wa mashtaka Bi Esther Kimani.

Bi Kimani alisema mkurugenzi wa mashtaka ya umma hapingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Hata hivyo alisema afisa huyo wa polisi anakabiliwa na shtaka mbaya la mauaji ambalo adhabu yake ni aidha kufungwa jela maisha ama kuhukumiwa kuuawa.

“Naomba ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia iwasilishwe hapa kortini kabla ya mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana,” Bi Kimani alisema.

Jaji Ogemba aliamuru mshtakiwa azuiliwe kwa muda wa wiki mbili ndipo ripoti hiyo ya afisa wa urekebishaji iwasilishwe kortini.

Bw Omari anayemwakilisha Mokamba alieleza mahakama kuwa mshtakiwa amemsihi aombe familia ya marehemu msamaha kwa “vile hakumuua kwa kukusudia. Ilikuwa bahati mbaya.”

Bw Omari alieleza mahakama kuwa Mokamba na Makuto walikuwa marafiki chanda na pete na kwamba hakukusudia kumuua.

“Mshtakiwa ameniomba niwasiliane na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma apunguziwe shtaka liwe la kuua bila ya kukusudia,” Bw Omari alisema.

Mshtakiwa huyo aliamriwa azuiliwe gereza la Industrial Area hadi ahojiwe na afisa wa urekebishaji tabia.

You can share this post!

CHOCHEO: Mume si suti, ni ujasiri!

Kalonzo amponda Ruto kwa kupinga wazo la urais wa mzunguko