Habari Mseto

Polisi alivyotumia gari la wenyewe alilokuwa akilinda kujipatia mkopo

April 17th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

WAPELELEZI wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kutoka kwa Kitengo cha Kuchunguza Uhalifu wa Kifedha, wanachunguza kisa ambapo polisi anadaiwa kutumia gari lililokuwa chini ya ulinzi wake kupata mkopo wa benki bila idhini ya mmiliki wa gari hilo.

Hati zilizowasilishwa kortini na afisa anayechunguza kisa hicho, Bw David Munga, zimefichua jinsi gari la Bi Lilian Bujede, lilitwaliwa na dalali wa kampuni ya upigaji mnada kwa mkopo ambao hakuwa na habari kuuhusu.

Mahakama imeelezwa kwamba, Bi Bujede alinunua gari hilo mwaka wa 2018. Miaka miwili baadaye, vipuri vya gari hilo viliibwa wakati likitumika katika biashara ya teksi.

Mwanamke huyo aliandikisha taarifa za wizi wa vipuri vya gari lake katika kituo cha polisi cha Mjambere, Mombasa.

Kesi hiyo ilikabidhiwa kwa mmoja wa maafisa katika kituo hicho kuchunguza kisa hicho, lakini inadaiwa alikataa kurudisha gari kwa mmiliki baada ya kumaliza uchunguzi.

Alimshawishi mtoto kumkabidhi cheti ya umiliki

Bi Bujede anadai kuwa, afisa huyo alizuru nyumbani kwake baadaye na kumshawishi mtoto wake kumkabidhi cheti cha kumiliki gari hilo bila ruhusa yake.

“Mwanamke huyo aliripoti kwa OCS wa Mjambere. Kisha alikadhidiwa gari hilo lakini bila stakabadhi hiyo kwani aliambiwa kuwa mchunguzi wa kesi hiyo alikuwa likizoni wakati huo,” alisema Bw Munga katika hati ya kiapo iliyowasilishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Mombasa, Bw David Odhiambo.

Katika mojawapo ya ziara zake katika kituo hicho cha polisi kufuatilia stakabadhi hiyo, inasemekana afisa huyo alimfahamisha mwanamke huyo waziwazi kwamba alitumia stakabadhi hiyo kama dhamana kupata mkopo wa Sh300,000 katika Benki ya Rafiki Microfinance.

Mnamo Agosti 2020, mwanamke huyo alipokuwa na gari lake Vihiga, anadai wafanyakazi kutoka kwa kampuni ya upigaji mnada ya MUMU walimwendea na maagizo ya kulitwaa kwa kukosa kulipia mkopo uliodhaminiwa na gari hilo.

“Gari hilo lilichukuliwa na madalali wa MUMU kutokana na mkopo ambao haukulipwa wa Sh377,170.15 uliopewa polisi huyo bila idhini ya mlalamishi,” akasema Bw Munga.

Bw Munga ameomba mahakama itoe amri zitakazomruhusu kupata stakabadhi muhimu kutoka kwa benki hiyo ili kuthibitisha madai ya mwanamke huyo.

Pia, mchunguzi huyo aliambia mahakama kuwa anachukulia tukio hilo kama kesi ya kupanga njama ya kufanya ulaghai.

Bw Munga pia anataka ruhusa ya kurekodi taarifa za wafanyakazi wa benki hiyo na stakabadhi nyingine yoyote au taarifa zinazohusiana na akaunti ya mkopo ya polisi huyo ambayo itasaidia katika uchunguzi.