Habari za Kitaifa

Polisi aliyemiminia raia risasi ‘katika hali ya kujikinga’ asukumwa jela miaka 15

February 2nd, 2024 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA afisa wa polisi aliyemuua mwanaume mwenye umri wa miaka 24 kwa kumtandika risasi tatu kifuani amehukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani.

Jaji Daniel Ogembo alimsukumia David Mwongera kifungo hicho baada ya kumpata na hatia ya kumuua Hemedi Majid mnamo Januari 16,2020.

Jaji Ogembo alisema Mwongera hakughairi makosa yake ila “alisisitiza alitekeleza uhalifu huo kwa kujikinga maana yeye na maafisa wa polisi wenzake wakijikinga walipovamiwa na vijana zaidi ya 20.”

Mshtakiwa pamoja na maafisa wa polisi wenzake walikuwa wameenda kusaka dawa za kulevya katika eneo la Majengo, Kamkunji, Nairobi.

Akijitetea, mshtakiwa alisema kundi la vijana waliwavamia na kuwatishia maisha ndipo wakapiga risasi angani kuwatawanya, lakini Hemed Majid na wenzake wakazidi kuwasogelea maafisa hao wa polisi ndipo alichapwa risasi kifuani na kichwani. Alifariki akipelekwa hospitalini.

Akipitisha hukumu, Jaji huyo alisema afisa huyo wa zamani katika kikosi cha polisi alitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya mwananchi ambaye hakuwa na silaha.

Alimpiga risasi Hemed kifuani na kichwani mtawalia.

“Mshtakiwa alimmiminia risasi tatu Hemed na kumuua papo hapo,” Jaji Ogembo alisema akipitisha hukumu.

Jaji huyo alisema ijapokuwa mshtakiwa amedai alikuwa anajikinga, hakuna ushahidi uliowasilisha kuthibitisha marehemu alikuwa na silaha yoyote kumwezesha “kuzamisha maisha yake kwa urahisi hivyo.”

Jaji huyo alisema silaha kamili dhidi ya kila afisa wa polisi ni kutenda haki na wala sio kutumia bunduki na bastola kwa njia mbaya.

Jaji Ogembo alisema mshtakiwa alitamatisha maisha ya Hemed Majid aliyekuwa tegemeo la mkewe na watoto.

Pia afisa huyo wa zamani wa polisi alielezwa “anastahili kifungo kikali ikitiliwa maana amekuwa gerezani tangu 2020.”

“Unahitaji kifungo cha gerezani utafakari matendo yako kisha upate fursa ya kujirekebisha,” Jaji Ogembo alimweleza mshtakiwa akipitisha adhabu.

Baada ya kusema hayo, Jaji Ogembo aliamuru mshtakiwa atumikie kifungo cha miaka 15 “kwa vile alitwaa maisha ya mtu.”

Alipewa siku 14 kukata rufaa.