Michezo

Polisi aliyemuua shabiki wa Arsenal taabani

January 28th, 2019 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

KAMATI ya Kushughulikia Malalamishi Dhidi ya Maafisa wa Polisi (IAU) imeanzisha uchunguzi kuhusu kisa ambapo afisa wa polisi anadaiwa kumpiga risasi na kumuua raia kutokana na kile walioshuhudia walisema ni kuhusiana na mechi kati ya Chelsea na Arsenal.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kamati, Bw Charlton Mureithi, faili ya uchunguzi imefunguliwa ambapo mashahidi wanawasilisha taarifa zao ili kubaini ukweli kuhusu mauaji ya Martin Mutheka anayedaiwa aliuawa na Konstebo Alfred Kasina.

Bw Mureithi alisema tayari afisa huyo amepokonywa bunduki ambayo imepelekwa kwa wataalamu ili kubaini ikiwa ndiyo iliyotumika katika mauaji ya Bw Mutheka.

Aliongeza kuwa idara yake inashirikiana na Tume ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) katika uchunguzi huo.

Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, afisa huyo alikuwa miongoni mwa mashabiki waliokuwa wakifuatilia mechi kwenye runinga katika baa moja wakati mzozo ulipozuka.

Kamanda wa polisi wa Kandara, Wilson Kosgey alisema watahakikisha ukweli umejulikana.

“Tukio hilo linachunguzwa na watu wasiwe na hofu kuwa tunapendelea afisa huyo. Ikiwa uchunguzi utampata na hatia, atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Kazi yetu haina nafasi ya utundu wa kiwango hicho,” akasema.

Mbunge wa Kandara, Bi Esther Wahome amesema atafuatilia suala hilo kwa makini ili kuhakikisha haki imetendeka.

“Mimi kama mbunge wa eneo hili na pia wakili, nitahakikisha haki imetendeka. Huwezi ukaja kazi hapa Kandara ya kuua kiholela watu wasio na hatia. Hakuna taarifa yoyote ya ushahidi hadi sasa ambayo imetolewa kuonyesha kuwa kijana huyo aling’ang’ana na afisa huyo. Pia hakuna wakati wowote kijana huyo aliweka maisha ya raia au ya afisa huyo katika hatari,” Bi Wahome akasema.