Habari

Polisi amuua mwenzake Kakamega

August 2nd, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

[email protected]

MAAFISA wa polisi wanachunguza kisa ambapo afisa mmoja katika Kaunti ya Kakamega alimuua polisi mwenzake kwa kumpiga risasi katika mtaa wa Milimani mjini Kakamega mnamo Alhamisi usiku.

Tukio hilo la saa moja na nusu usiku lilihusisha afisa Philip Wahome chini ya APS CIPU aliyekuwa akidumisha usalama katika dukakuu la Khetias alitofautiana na mwenzake aliyetambuliwa kwa jina Philemon Kipkoech, 24, ambapo alimmiminia risasi.

Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Kakamega Bernard Muli amesema hawajabainisha ni nini hasa kilijiri.

“Hatujabainisha hasa sababu ya farakano kati yao,” amesema Muli akieleza kwamba mhanga alipigwa risasi mgongoni akafariki papo hapo.

Afisa huyo alifariki bunduki aina ya AK47 ikiwa mkononi.

 

Maiti imepelekwa katika Hospitali Kuu katika Kaunti ya Kakamega.