Habari Mseto

Polisi ange kuzima njama za kigaidi

June 9th, 2019 1 min read

Na MARY WAMBUI

MAAFISA wa polisi nchini wako macho kutokana na uwezekano wa kutokea kwa shambulizi la kigaidi kufuatia kukamatwa kwa washukiwa wanne wa ugaidi katika hoteli za Intercontintal na Hilton, Nairobi mnamo Jumanne na Alhamisi.

Vilevile kitengo cha usalama kiliripoti kwamba vilipuzi na zana hatari zilipatanikana Ijumaa iliyopita katika barabara kuu ya Narok-Bomet, hali inayozidisha hatari ya kiusalama.

Mnamo Jumanne, washukiwa wawili walikamatwa katika hoteli ya Hilton baada ya mienendo yao kuzua maswali huku wengine wawili wenye asili ya Kisomali pia wakinyakwa katika hoteli ya Intercontinental walikoenda kama wageni waliotaka kukodi chumba ilhali hawakuwa na stakabadhi maalum.

Akizungumza na Taifa Leo, Mkuu wa Polisi wa Nairobi Phillip Ndolo alisema maafisa wa usalama wamewekwa katika hali ya tahadhari kuhusu shambulio la kigaidi hata baada ya kukamilika kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan, wakati ambao onyo kuhusu matukio ya kigaidi lilitolewa.

“Onyo tulilolitoa bado linabakia hivyo na litaendelea kwa muda. Hata hivyo, halifai kuzingatiwa katikati mwa jiji pekee bali pia katika maeneo mengine nchini,” akasema Bw Ndolo.

Washukiwa walionyakwa wanaendelea kuhojiwa kuhusu mienendo yao katika vituo mbalimbali vya polisi ambavyo Bw Ndolo hakuvifichua kutokana na sababu za kiusalama.

“Uchunguzi bado unaendelea na huenda ukachukua muda zaidi. Hakuna aliye na stakabadhi za utambulisho kati yao na tunataka kujua walitoka wapi, walikuwa wakienda wapi na lengo lao lilikuwa nini,” akaongeza Bw Ndolo kuhusu washukuwa waliobambwa Nairobi.

Ingawa hivyo, alisema wanne hao huenda wasifunguliwe mashtaka ya kupanga shambulizi la kigaidi lakini watakabiliwa kisheria kutokana na makosa mengine punde tu uchunguzi utakapokamilishwa.

Kufuatia matukio hayo mawili jijini Nairobi, polisi walizidisha doria Jumamosi na Jumapili jijini humo na maeneo ya kuabudu.

Akizungumza akiwa Bomet, Msemaji wa Polisi Charles Owino alisema kuwa maafisa wa polisi siku za nyuma wametibua njama nyingi za kigaidi kwa sababu Wakenya wamekuwa wakiwapasha habari kuhusu watu wenye mienendo ya kutiliwa shaka.