Kimataifa

Polisi asukumwa jela kwa kumpiga risasi na kumuua mvulana Mwafrika

August 30th, 2018 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

CHICAGO, MAREKANI

MAHAKAMA moja ya Texas Jumanne ilimpata afisa mzungu na makosa ya mauaji ya mvulana mweusi wa miaka 15, kwa kumpiga risasi.

Korti ilielezwa Roy Oliver alipiga risasi tano katika gari lililojaa vijana matineja mwaka uliopita, akiishia kumuua Jordan Edwards, mvulana mwenye asili ya kiafrika.

Afisa huyo alidaiwa kufanya hivyo baada ya kufahamishwa kuhusu kisa cha watoto wasiofikisha miaka iliyoruhusiwa kunywa pombe kuwa walikuwa wakilewa katika sherehe eneo la Dallas.

Edwards pamoja na wenzake wanne walikuwa wakiondoka kwenye sherehe hiyo baada ya kusikia milio ya risasi, iliyotokea eneo jirani. Korti ilielezwa Oliver alipiga risasi kwenye gari la matineja hao, ikimpata marehemu kichwani.

Korti hiyo hata hivyo ilimwondolea makossa ya mateso afisa huyo, ambaye alishafutwa.

Sasa afisa huyo wa zamani ako kwenye hatari ya kupokea kifungo cha hadi miaka 99 baada ya kuhukumiwa kwa kosa hilo la mauaji.

Wazazi wa mvulana aliyeuawa walitokwa na machozi ya furaha baada ya uamuzi wa korti wakisema hatimaye haki imepatikana.

“Nina furaha, furaha sana. Umekuwa muda mrefu,” akasema babake marehemu, Odell Edwards.

Familia hiyo iliambia gazeti moja la Marekani kuwa kesi hiyo ni ya umuhimu kwa Waafrika wote walio Marekani ambao wameuawa bila hatia na familia zao bado hazijapata haki.

Polisi huyo mbeleni alijitetea kuwa alipiga risasi kwa kuwa gari hilo lilikuwa likimkaribia kwa kasi lakini akabadili hadidhi baada ya kanda iliyoonyesha gari hilo likiendeshwa kuelekea mbali naye kuonyeshwa korti.

Japo kwenye ushahidi wa kortini alisema sababu ya kupiga risasi ni kwa kuwa gari la vijana hao lilikuwa likiendeshwa kuelekea kwa afisa mwenzake Tyler Gross na hivyo kuhatarisha maisha yake, Gross alieleza korti kuwa hakuhisi maisha yake kuwa hatarini wakati wowote ule.

“Niliwataka tu kusimama, sikuwa na woga wakati huo,” Gross akaeleza korti.

Kisa hicho kilikuwa kimoja kati ya vingi ambavyo maafisa wazungu waliwauwa watu wa asili ya kiafrika.