Habari Mseto

Polisi atetea hatua ya kumpiga mshukiwa wa uhalifu risasi kichwa na mkononi

May 30th, 2024 1 min read

NA BRIAN OCHARO

AFISA wa polisi ametetea hatua yake ya kumpiga risasi mwanamume katika eneo la Likoni mnamo 2018 alipokuwa akitafuta magenge ya wahalfu.

Konstebo wa polisi, Yunus Athman, alifahamisha mahakama kwamba alikuwa akijikinga dhidi ya mshukiwa wa uhalifu aliyekuwa na panga.

Alimweleza Jaji Ann Ong’injo kwamba alimpiga Mbaraka Maitha Omar risasi mbili, mkononi na kichwani. Bw Athman alikanusha kuhusika kwa vyovyote katika kupanga mauaji ya marehemu.

“Ilikuwa ni wakati wa hofu, sikuwahi kukumbana na hali kama hiyo hapo awali. Nilimpiga risasi ili kumkamata. Nilitaka atupe upanga chini ili nimkamate; hiyo ndiyo ilikuwa nia yangu. Maisha yangu na ya watu wengine wawili niliokuwa nao yalikuwa hatarini,” alieleza.

Anadaiwa kutenda kosa hilo mnamo Septemba 10, 2018 katika kijiji cha Mwanza, Likoni.

Kupitia kwa wakili wake Eugene Wangila, Bw Athman alieleza kuwa hakuwa akifahamiana na marehemu kabla ya kisa hicho na aliongozwa hadi kwenye makazi ya Bw Omar na mdokezi.