Habari MsetoMichezo

Polisi aua raia Murang'a kwa hasira za Chelsea kupigwa na Arsenal

January 24th, 2019 2 min read

Na NDUNG’U GACHANE

MWANAMUME alifariki Alhamisi baada ya kupigwa risasi mara tatu na afisa wa polisi aliyekasirika baada ya timu anayoshabikia ya kandanda kushindwa Jumapili iliyopita.

Bw Martin Waweru kutoka kijiji cha Muruka, eneobunge la Kandara katika Kaunti ya Murang’a, alipigwa risasi na afisa wa AP anayefanya kazi katika kambi ya Muruka alipokuwa akienda nyumbani kutoka baa walimokuwa wakinywa pombe na kutazama mechi ya kandanda.

Inasemekana afisa huyo wa polisi alikasirika baada ya timu anayoshabikia ya Chelsea kushindwa na Arsenal mabao 2-0.

Marehemu, aliyezungumza na Taifa Leo mnamo Jumatano jioni kabla kufariki jana asubuhi, alieleza kwamba alikuwa amefika kijijini ambako alikuwa akifanya kazi ya kusambaza mitungi ya gesi, na akaamua kujiburudisha kwa pombe ndipo alipokutana na afisa huyo pamoja na wanakijiji wengine wakitazama mechi.

Alisema baada ya kunywa glasi mbili za pombe ya Keg, aliamua kwenda nyumbani kwa mke wake na binti na akawanunulia mkate na samaki.

Alipokuwa akiondoka kulikuwa na kizaazaa kati ya polisi huyo na wanakijiji baada ya timu ya Chelsea kushindwa.

Marehemu alisema alianza safari yake ya nyumbani lakini afisa akampita na kwenda moja kwa moja hadi kambini, kisha akamwona akirudi akiwa na bunduki. Wakati huo wanakijiji wengine pia walikuwa nyuma yake wakielekea nyumbani.

“Alipofika mahali nilipokuwa aliniagiza nilale chini nikamtii, kisha akanipiga risasi mara tatu kutoka nyuma kiunoni, mgongoni na mkononi, kisha akanivuta hadi kambini akanilazimisha kunywa maji nilipokuwa nikivuja damu nyingi,” akasema.

Aliongeza: “Wanakijiji walijaribu kunisaidia lakini hawangeweza kwa kuwa afisa huyo na wengine wawili waliwazuia kunipeleka hospitalini wakisisitiza lazima nipelekwe kwa gari la polisi.”

Afisa Mkuu wa Polisi eneo la Kandara, Bw Wilson Kosgey alisema wameanzisha uchunguzi na wanasubiri pia Mamlaka Huru ya Utendakazi wa Polisi (IPOA) ianzishe uchunguzi wake.

“Tumeanzisha upelelezi kuhusu suala hilo na tunaalika IPOA iingilie kati lakini uchunguzi wa mapema unaonyesha hapakuwa na sababu ya kufanya mwanamume huyo apigwe risasi kwani hakuwa na hatari yoyote kwa afisa wa polisi,” akasema.