Polisi chonjo kukabili magenge msimu huu

Polisi chonjo kukabili magenge msimu huu

Na WAANDISHI WETU

POLISI katika maeneo ya Pwani wametoa onyo kali kwa magenge ya wahalifu na wafadhili wao wakati nchi inapoelekea kwa msimu wa sherehe za Desemba na vile vile Uchaguzi Mkuu.

Imebainika kuwa, mikakati ya kiusalama imezidishwa kwa vile inaaminika wahalifu hutumia sana misimu hiyo miwili ambayo mwaka huu inafuatana, kutatiza amani.Katika Kaunti ya Mombasa, maeneo ya Likoni, Kisauni na Nyali, yalitajwa kuwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa usalama.

Imefichuka magenge ya uhalifu tayari yameanza kuchipuka tena, na mengi yanahusishwa na utumizi wa dawa za kulevya.Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko, alilalamika kuhusu genge ambalo lina watoto wa kati ya umri wa miaka 12 hadi 17.“Eneo langu lina tatizo la kiusalama kwa sababu ya matumizi ya mihadarati. Magenge ya vijana yanachipuka kila siku.

Kuna genge hatari linajulikana kama Chafu ambalo linaongozwa na mtoto wa miaka 13. Mtoto anawezaje kuongoza genge la wahalifu?” akauliza.Kamishna wa eneo la Pwani, Bw John Elungata, alihakikishia viongozi na wakazi kwamba serikali imejitolea kukabiliana na mihadarati ili kudumisha usalama katika ukanda huo.

Katika Kaunti jirani ya Kilifi, wakuu wa idara ya polisi, walisema mikakati imeongezwa kuhakikishia wakazi usalama.Maeneo ya Mtwapa, Chumani, Tezo, Matsangoni, Watamu na Mambrui, yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama.

Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Kilifi, Bw Kutswa Olaka, alisema visa vya ukosefu wa usalama vimepungua sana katika eneo hilo na wamenuia kuhakikisha hali itaendelea kuwa shwari kwa manufaa ya wakazi na wageni.“Ile mikakati ambayo ilikuwepo bado iko, na tumeongeza mingine ambayo hatutasema kwa sasa.

Lakini nataka kuhakikishia wananchi kuwa usalama wao uko imara,’ akasema, katika mahojiano na Taifa Leo.Wakuu wa polisi katika Kaunti ya Kwale pia walisema kuwa maafisa wa kutosha watatumwa kwa hoteli, mitaa, barabarani na maeneo yoyote ambayo yatakuwa na tishio la usalama.

Hivi majuzi, kaunti hiyo iliongeza operesheni za usalama kwenye barabara kuu ya Likoni-Lungalunga ambapo maafisa wa jeshi la ulinzi wa taifa (KDF) walihusishwa.Maafisa hao walikuwa wakikagua vibali vya kuingia nchini na vitambulisho vya kitaifa katika sehemu za barabara hiyo.

Kamishna wa Kaunti hiyo, Bw Gideon Oyagi, alisema maafisa wa polisi wameagizwa kuwa macho ili kuzima tishio lolote la ukosefu wa usalama.Sehemu zinazotiliwa maanani zaidi ni katika ufuo wa bahari wa Diani, Lungalunga katika mpaka wa Kenya na Tanzania, na pia katika hoteli hasa kaunti ndogo ya Msambweni.

“Tumeongeza ulinzi ndani na nje ya mipaka yetu ili kuhakikisha likizo ya amani na salama kwa wenyeji na wageni wanaotarajiwa kuja. Tutahakikisha polisi wamepiga doria katika kaunti nzima hasa katika maeneo yatakayokuwa na watu wengi,” Bw Oyagi alisema.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia, aliambia Taifa Leo, maafisa wa kutosha wa usalama wamesambazwa kushika doria kwenye vizuizi vya barabarani na pia sehemu za mpakani mwa Kenya na Somalia na zile za msitu wa Boni.

Kamishna huyo aliorodhesha maeneo ya Mkomani katika kisiwa cha Lamu na yale ya Lamu Mashariki, ikiwemo Mbwajumwali, Tchundwa, Faza, Kizingitini miongoni mwa mengine yatakayoangaziwa zaidi na idara ya usalama.

“Kivyovyote vile sisi tuko imara kuona kwamba amani inadumishwa maeneo hayo,” akasema Bw Macharia.Ripoti za Winnie Atieno, Maureen Ongala, Siago Cece na Kalume Kazungu

You can share this post!

Betis yapiga breki rekodi nzuri ya kocha Xavi kambini mwa...

OKA, Raila wataungana kukabili Ruto 2022 – Lenku

T L