Polisi Kamukunji wachunguza kilichosababisha moto katika bweni

Polisi Kamukunji wachunguza kilichosababisha moto katika bweni

Na SAMMY KIMATU

MAJASUSI katika kaunti ndogo ya Kamukunji wanachunguza chanzo cha moto ulioteketeza bweni moja katika shule moja ya upili ya wasichana wiki jana.

Kisa hicho kilitokea mnamo Alhamisi iliyopita saa moja za asubuhi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St Anne iliyoko mkabala wa barabara ya Jogoo katika kaunti ndogo ya Kamukunji. Akizungumza jana, Kamanda wa Kitengo cha Ulinzi wa Majumba yenye Afisi za Serikali eneo la Makadara (CIPU) Bw James Kariuki alisema moto ulianza kutoka kwa chumba kimoja kabla ya kusambaa hadi kwenye bweni yote.

Kando na hayo bweni hilo lina vitanda 112 za wanafunzi kutoka kila kidato. Mali ya thamani isiyojulikana iliharibiwa na moto.

Bw Kariuki alieleza kwamba maafisa wake wanafanya kazi saa 24 kubaini chanzo cha moto.

Aliongeza kwamba hadi jana, bado hawajafahamu kilichosababisha moto.

”Kufikia jana, bado maafisa wetu wa polisi wanachunguza kilichosababisha moto katika St Anne’s Girls wiki jana. Hata hivyo, maafisa wangu wanafanya kazi usiku na mchana hadi wabaini chanzo cha moto,’’ Bw Kariuki akaambia Taifa Jumapili.

Bw Kariuki aliongeza kwamba wanafunzi walioshtuka kwa sababu mali zao ziliteketezwa walipelekwa katika Kituo cha Afya cha Makadara.

Vile vile, Bw Kariuki alidokeza kwamba magari ya kuzima moto kutoka Idara ya kushugulikia Huduma ya Jiji la Nairobi wakisaidiwa na wananchi walifanikiwa kuuzima moto huo.

Hata hivyo, hakuna majeruhi walioripotiwa kwenye kisa hicho.

  • Tags

You can share this post!

Mjane wa balozi wa Italia nchini DRC avunja kimya

Niliwahi kujaribu kumsajili Bruno Fernandes wa Manchester...