Habari za Kaunti

Polisi Kisii wanasa bangi ndani ya magari manne

April 24th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

POLISI mjini Kisii wamenasa bangi ya thamani ya Sh37 milioni na kufanikiwa kumkamata mshukiwa mmoja.

Mshukiwa huyo Joseph Ouma, alikamatwa Jumanne usiku katika eneo la Itierio, kwenye barabara ya Kisii-Migori lakini washirika wenzake walikwepa mtego wa polisi na kuingia mafichoni.

Kulingana na ripoti ya polisi ambayo Taifa Leo imeona, bangi hiyo ilikuwa ikisafirishwa katika msafara wa magari manne.

Magari yaliyohusika ni Probox mbili, Toyota Hiace na gari la matatu Nissan. Gari aina ya Toyota Hiace lilikuwa linafanana na la kampuni moja ya mawasiliano humu nchini.

“Mnamo Jumatano, mwendo wa saa mbili usiku, maafisa kutoka vitengo mbalimbali kikiwemo cha kukabiliana na uhalifu wa kimataifa kilicho katika makao makuu ya DCI Nairobi na maafisa kutoka Kituo cha Polisi cha Gesonso, waliufuata msafara wa magari manne kwenye ya Migori-Kisii na kuwazuia walanguzi wa bangi katika eneo la Itierio,” ilisoma sehemu ya ripoti ya polisi.

Baada ya kugundua kwamba polisi walikuwa wakiwaandama, mmoja wa madereva wa probox alikimbia.

Hili liliwafanya polisi kulifyatulia risasi gari lake kwa lengo la kutoa pumzi tairi za gari hilo lakini dereva huyo aliruka nje na kutokomea eneo lisilojulikana.

Maafisa hao walifanikiwa kumkamata dereva mmoja ambaye pia alikuwa akiendesha gari jingine aina ya Probox. Katika gari lake, kilipatikana kibunda cha Sh30,000, pesa ambazo polisi wanaamini zilitokana na biashara hiyo haramu nchini.

Magari yaliyotelekezwa yalivutwa hadi Kituo cha Polisi cha Gesonso.

Mmojawapo wa washukiwa waliokuwa na bangi iliyonaswa katika eneo la Itierio, kwenye barabara ya Kisii-Migori ikisafirishwa kwa magari manne. PICHA | PICHA | WYCLIFFE NYABERI

Baada ya uchunguzi wa kina, ilibainika walikuwa wakisafirisha magunia 50 yaliyokuwa na vifagio ya bangi kavu ambayo thamani yake ya mitaani ilikuwa Sh37 milioni.

Ripoti ya polisi pia ilifichua kuwa mshukiwa huyo atahamishwa hadi makao makuu ya DCI kwa uchunguzi zaidi.

Visa vya polisi kunasa bangi kwenye hiyo ya Kisii-Migori si jambo jipya. Aghalabu mwezi hauwezi kuisha bila kesi kama hizo kuripotiwa.

Inashukiwa kwamba bangi hiyo iliingizwa nchini kinyemelea katika mpaka wa Kenya na Tanzania.

Katika visa vingine, baadhi ya maafisa wa polisi wanasemekana kuhusika katika kuwalinda wale wanaouza bangi kwa vile wao pia wana maslahi fulani katika biashara hiyo.

[email protected]