Habari Mseto

Polisi kizimbani kwa kumumunya mamilioni ya NSSF

July 6th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wakuu wawili wa polisi akiwamo naibu wa afisa msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Narok (OCS) walishtakiwa Jumatatu kwa kulaghai Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) Sh3.4 milioni.

Bw Milton Odhiambo Barasa, aliye naibu wa OCS na James Thuo Njuguna, wa kitengo cha kupiga picha walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bi Martha Mutuku.

Walikanusha shtaka la kula njama za kumumunya hela za malipo ya uzeeni ya kikosi cha polisi Sh3,482,451 kwa kuidhinisha hati feki za Samuel Kiprotich Bett.

Washtakiwa hao walidaiwa walitekeleza uhalifu huo kati ya 2017 na 2018 katika makao makuu ya polisi jijini Nairobi.

Shtaka la pili lilisema hawakuchukua tahadhari iwapasavyo kuzuia kutoweka kwa pesa hizo..

Washtakiwa waliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana wakifichua wamehudumia kikosi cha polisi kwa zaidi ya miaka 27 kila mmoja na “ wanaendelea kutekeleza majukumu yao.”

Mahakama ilifahamishwa washtakiwa walipigiwa simu kutoka stesheni wanakohudumu kufika katika makao makuu ya uchunguzi (DCI) kuhojiwa.

“Washtakiwa walizuiliwa tangu Ijumaa hadi leo walipofikishwa kortini,” hakimu alielezwa.

“Huduma za washtakiwa zingali zahitajiwa hasa wakati huu wa kupambana na ugonjwa wa Corona na visa vingine vya uhalifu,” Bi Mutuku alielezwa na wakili anayewatetea washtakiwa hao.

Hakimu aliwaamuru washtakiwa hao walipe kila mmoja dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu.

Pia aliwataka wafike kortini tena Julai 20, 2020 kutengewa siku ya kusikizwa kwa kesi inayowakabili.