Habari Mseto

Polisi kuchunguza zaidi dereva aliyenaswa na Sh1m akielekea Ethiopia

June 4th, 2019 1 min read

Na WAWERU WAIRIMU

MAHAKAMA ya Isiolo imewapa polisi wiki moja kumaliza uchunguzi katika kesi ambapo dereva mmoja wa Serikali ya Kaunti ya Samburu alikamatwa akiwa na Sh1 milioni katika barabara kuu ya Isiolo-Moyale.

Dereva huyo, aliyetambuliwa kama Samuel Lekisaat alikamatwa mnamo Jumamosi pamoja na watu wengine wawili; Joseph Lekakuli na Philip Lekisaat wakisafirisha fedha hizo katika gari aina ya Toyota Fortuner, lenye nambari za usajili 25CG 032A.

Gari hilo linamilikiwa na Wizara ya Huduma za Jamii katika kaunti hiyo.

Gari lilinaswa na kundi la maafisa wa usalama ambao walikuwa wakifanya ukaguzi katika magari katika barabara hiyo. Maafisa hao walipata Sh1, 099, 000 zikiwa zimefungwa katika karatasi nyeusi.

Mnamo Jumatatu, watatu hao walifikishwa mbele ya Mahakama ya Isiolo, lakini upande wa mashtaka ukaomba muda wa siku kumi kuchunguza akaunti za washukiwa hao watatu. Kiongozi wa Mashtaka, Bw Joseph Mburugo, alipinga washukiwa hao kuachiliwa kwa dhamana, akisema kuwa wanaweza kuingilia uchunguzi.

“Tunaomba muda zaidi kumaliza uchunguzi wetu,” akasema Bw Mburugo.

Hakimu Mkuu Joseph Mungai alikubali ombi hilo, akiwapa polisi siku saba kumaliza uchunguzi wao.

“Nimekubali ombi la upande wa mashtaka. Ninaamini kuwa upande wa mashtaka unahitaji muda zaidi kumaliza uchunguzi wake,” akasema. Mahakama iligiza watatu hao kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Wamba.

Kulingana na polisi, huenda washukiwa wakafunguliwa mashtaka ya wizi na ulanguzi wa pesa.