Habari Mseto

Polisi kukamatwa kutoa ushahidi katika kesi ya ugaidi

April 22nd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA moja ya Mombasa Ijumaa iliamuru maafisa wawili wa polisi kutoka kitengo cha kupambana na ugaidi watiwe nguvuni kwa kukosa kufika kortini kutoa ushahidi dhidi ya wanawake wanne wanaokabiliwa na shtaka la kuwa wanachama wa kundi la magaidi wa Al Shabaab.

Akitoa kibali cha kuwakamata , hakimu mkuu Bw Evans Makori alisema amekuwa akiwatahadharisha maafisa wa polisi wanaochunguza kesi dhidi ya kuzembea kazini mwao.

“Maafisa wa polisi wanaochunguza kesi kaunti ya Mombasa wamekuwa mwimba katika utenda kazi wa mahakama na wahusikao sharti waadhibiwe,” alisema Bw Makori.

Hakimu huyo alisema mara nyingi kesi zimekuwa zikitupiliwa mbali kutokana na sababu za maafisa wa polisi waliochunguza kesi kufika kortini kutoa ushahidi ama kukosa kuwasilisha ushahidi.

Alisema uzembe wa maafisa wanaochunguza kesi wa kutowasilisha ushahidi ni njia moja ya kuvuruga  utenda kazi wa mawakili, kuwatesa washukiwa na vile  kusababisha mahakama kuchelewesha kuamua kesi katika muda unaofaa.

“Namwamuru afisa anayesimamia kitengo cha ATPU eneo la Pwani Bw Charles Ogeto awakamate na kuwafikisha kortini Koplo Samuel Ouma na Konstebo Fogat Abdi waeleze sababu ya kutotoa ushahidi dhidi ya washukiwa hawa wanne,” hakimu aliamuru.

Bw Makori pia alimwagiza OCPD Mombasa asaidie katika kutiwa nguvuni kwa maafisa hao wawili wa polisi.

Maafisa hao walikuwa wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi dhidi ya Bi Ummulkheir Sadri Abdalla , Bi Khadija Abubakar Abdulkadir, Bi Maryam Said Aboud na Bi Halima Adan wanaoshtakiwa kuwa wanachama wa Al-Shabaab.