Habari

Polisi kulinda Sossion afisini

September 21st, 2019 2 min read

Na MAUREEN KAKAH na BENSON MATHEKA

KATIBU Mkuu wa chama cha walimu (Knut), Wilson Sossion, sasa atakuwa akilindwa na maafisa wa polisi akiwa kazini katika afisi za chama hicho katikati ya jiji la Nairobi.

Mahakama iliagiza Mkuu wa Polisi eneo la katikati mwa jiji (OCPD), afisa anayesimamia kituo cha polisi cha Kamukunji (OCS) na maafisa wengine wa usalama kuhakikisha kwamba Bw Sossion amefika, kuingia na kufanyakazi katika ofisi za chama zilizoko barabara ya Mfangano bila kutatizika kwa vyovyote vile.

Huu ni ushindi mkubwa kwa Bw Sossion ambaye alizuiwa kuingia katika afisi hizo na kundi la maafisa wanaodai kwamba walimuondoa mamlakani.

Maafisa hao waliapa kutomruhusu Bw Sossion kukanyaga katika afisi hizo wakisema, uamuzi wao ulikuwa wa mwisho na kwamba, nafasi ya katibu huyo ilikuwa imechukuliwa na mtu mwingine.

Jana, Jaji Maureen Onyango alikubali ombi la Bw Sossion na kuagiza polisi wamsindikize na kuhakikisha ameingia katika afisi hizo.

Katika ombi la dharura mbele ya Mahakama ya Leba, Bw Sossion alitaka mahakama iagize apatiwe ulinzi ili aweze kufika katika afisi za chama. “Mkuu wa polisi eneo la Nairobi (OCPD), OCS wa Kamukunji au afisa mwingine anayehusika ameagizwa kumsaidia Bw Sossion kufika katika afisi yake na kumpa ulinzi unaofaa akiwa katika ofisi hizo,” Jaji Onyango alisema.

Kwenye ombi lake, Bw Sossion alikuwa ameomba aruhusiwe kuingia katika ofisi hizo hata kama ni kwa kuzivunja mradi tu aandamane na maafisa wa polisi.

Hata hivyo, mahakama haikukubali ombi hilo na badala yake ikaagiza asindikizwe na kulindwa akiwa kazini.

Mapema mwaka huu, Bw Sossion alipinga hatua ya msajili wa vyama vya wafanyakazi ya kufuta jina lake kama katibu mkuu wa Knut akisema, Baraza la Kitaifa la chama hicho lilimuondoa kinyume cha sheria.

Alisema kwamba, mkutano uliodaiwa kumuondoa haukuwa halali kwa sababu alikuwa na agizo la mahakama kuusimamisha.

Bw Sossion ambaye ni mbunge wa kuteuliwa wa chama cha ODM, amekuwa akipigwa vita na baadhi ya wanachama wa NEC tangu alipotofautiana na Tume ya Walimu (TSC) kuhusu muafaka wa nyongeza ya mishahara wa 2017 -2021 ambao walimu walitaka wapatiwe nyongeza ya jumula ya mishahara ya Sh54 bilioni.

Kumpiga vita

Ameshtaki wanachama 27 wa NEC wakiongozwa na mwenyekiti Wycliff Emuchei ambao wameungana kumpiga vita.

Katika kesi nyingine, Jaji Hellen Wasilwa wa Mahakama ya Leba ataamua wiki ijayo ikiwa katibu huyo ataondolewa afisini au ataendelea kushikilia wadhifa wake. Jaji Wasilwa alitoa agizo la kumzuia kufurushwa hadi kesi ambayo wapinzani wake walifichua alivyotimuliwa itaamuliwa.

Wapinzani hao wanasema kwamba, alienda kortini kuzuia mkutano ambao tabia yake ingejadiliwa. Kulingana na maafisa hao, lengo la Sossion lilikuwa ni kulemaza shughuli za chama.

Wanataka azuiwe kuhudumu kama Katibu Mkuu wa chama cha Knut na kuzuiwa kutoa pesa kutoka akaunti za chama hicho kikubwa cha walimu nchini.

Mnamo Machi, Sossion alizuiwa kuingia katika afisi hizo na watu aliodai ni wakora waliolipwa na wapinzani wake.