Habari Mseto

Polisi lawamani kuachilia 'probox' ya TZ iliyonaswa kwa wizi

February 4th, 2019 1 min read

NA VITALIS KIMUTAI

MAAFISA wa polisi wa ngazi za juu mjini Bomet wameshutumiwa vikali na wananchi kwa kuachilia gari lenye nambari ya usajili ya Tanzania lililonaswa na wadogo wao huku visa vya wizi wa magari vikiendelea kukithiri jijini humo.

Gari hilo lilinaswa baada ya dereva wake aliyedai analimiliki kukosa kutoa stakabadhi za kuunga madai yake, wakati ambapo idadi ya magari yaliyopotea mjini Bomet ikipanda hadi 11 katika muda wa miezi miwili iliyopita.

Nambari ya usajili ya gari hilo aina ya Toyota Probox T928BSH ilikuwa imevurugwa, gari lenyewe halikuwa na bima huku dereva akikosa kutoa cheti cha muda cha kuliruhusu kuingia nchini kutoka kwa idara ya uhamiaji mpakani.

Maafisa wa polisi wa trafiki walilinasa majuma mawili yaliyopita katika eneo la Kyogong kwenye barabara ya Bomet-Mulot na kulifikisha katika kituo cha polisi cha Bomet. Baadaye dereva huyo aliachiliwa kwa dhamana ya Sh6,000 pesa taslimu katika kituo hicho bila kufikishwa mahakamani.

Hata hivyo, hatua ya maafisa wa cheo cha juu kuachilia gari hilo siku ya Ijumaa ilizua ghadhabu za wafanyabiashara na umma ambao wamekuwa wakifuatilia tukio hilo kwa makini.

Maswali zaidi yameibuka kwa nini gari hilo liliachiliwa siku ambayo OCPD Samson Rukunga aliyehamishwa hadi Kituo cha Polisi cha Kiganjo alipokuwa akimkabidhi usukani mrithi wake George Walumbe.

Ingawa hivyo, Bw Walumbe alisema kwamba hafahamu chochote kuhusu utata huo na kuahidi kutoa taarifa baada ya kuwasiliana na OCS Daniel Nyagako na kupata ufafanuzi wa kuridhisha.

Polisi wamekuwa wakilaumiwa kwa kulegea na kushirikiana na wezi ili kufanikisha wizi wa magari ya kibinafsi yanayoegeshwa mjini Bomet.