Habari Mseto

Polisi lawamani kwa kuua vijana maskini kiholela

July 3rd, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KWA mara nyingine, polisi wamelaumiwa kwa kuwaua kiholela vijana kutoka mitaa masikini jijini Nairobi wakiwahusisha na madai ya uhalifu.

Kulingana na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, kuanzia Agosti 2018, polisi wamewaua wanaume na vijana 21 katika mitaa ya Mathare na Dandora jijini Nairobi.

“Mauaji haya ya kiholela yanaonyesha kuna shida kubwa zaidi ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi wakidai kwamba wanadumisha usalama katika mitaa ya mabanda jijini Nairobi na kukataa kufuata sheria ili kuhakikisha mauaji yanayotekelezwa na maafisa wa polisi yanachunguzwa,” HRW ilisema kwenye taarifa.

Mtafiti mkuu wa shirika hilo barani Afrika, Otsieno Nyamwaya, alisema kwamba polisi hawasaidii shirika huru la kuchunguza utendakazi wa polisi (IPOA) kuchunguza visa hivyo ili kuhakikisha wanaohusika wanachukuliwa hatua.

“Polisi wanawakamata watu ambao hawana silaha na kuwaua kwa kuwapiga risasi na huduma ya polisi au shirika la kuchunguza utendakazi wa polisi hawafanyi chochote kusimamisha mauaji haya,” alisema Bw Nyamwaya.

Afisa huyo anasema kwamba mauaji hayo yanapaswa kuchunguzwa na maafisa wanaoyatekeleza kuchukuliwa hatua za kisheria

Anasema polisi huwa hawaripoti visa vya mauaji ya kiholela au kuanza utaratibu wa kuyachunguza inavyohitajika kisheria.

Msemaji wa polisi, Charles Owino, alisema IPOA inapaswa kuchunguza visa vya mauaji ya kiholela vinavyotekelezwa na maafisa wa polisi.

“Afisa yeyote wa polisi anayekiuka sheria anapaswa kuchukuliwa hatua binafsi. Katika mauaji ya Mathare na Dandora, IPOA inafaa kufanya uchunguzi na kuhakikisha waliohusika wanashtakiwa,” alieleza Bw Owino.

Hata hivyo, HRW inasema kwamba makamanda wa polisi wanaosimamia maafisa wanaotekeleza mauaji hayo hawachukui hatua zozote kuwaadhibu.

“Mauaji haya yanafanyika na makamanda wa polisi wanaosimamia maafisa hao hawachukui hatua kuyazuia au kuwaadhibu wanaohusika,” alisema Bw Nyamwaya.

Kulingana IPOA, polisi huwa hawatayarishi ripoti za kuhusu mauaji hayo ambazo shirika hilo linaweza kutumia kuanza uchunguzi.

Shirika hilo pia lina nguvu za kisheria za kuanza uchunguzi huru kuhusu vitendo vya maafisa wa polisi.

Kulingana na maafisa wa IPOA waliozungumza na HRW, wachunguzi wake hugonga mwamba wakichunguza visa vya mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na polisi kwa sababu mashahidi huwa wanaogopa kuwapa habari muhimu.

Lilimnukuu Bw Owino akitetea maafisa wa polisi katika mitaa ya Dandora na Mathare kwa kusema wamekuwa wakichukua hatua za kulinda umma dhidi ya wahalifu.