Habari

Polisi mafisi

December 16th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

VISA vya maafisa wa polisi kushambulia watoto wa kike na kuwanajisi vimeongezeka katika maeneo tofauti ya nchi siku za karibuni.

Katika kipindi cha wiki moja pekee, kumeripotiwa visa visivyopungua vitano ambapo watoto wa umri kati ya miaka 13 na 16 walinajisiwa na maafisa wa polisi.

Katika baadhi ya visa hivyo, watoto hao walikuwa wameenda kutafuta usaidizi kwa polisi bila kujua walikuwa wanajiingiza midomoni ya fisi.

Jumamosi, afisa wa polisi katika Kituo cha Naromoru, Kaunti ya Nyeri alikamatwa kwa madai ya kumnajisi mtoto wa miaka 13 kituoni Ijumaa jioni.

Ripoti ya polisi ilionyesha Konstebo Stephen Wachira alimshambulia mtoto huyo aliyepelekwa kituoni na wasamaria wema ambao walimpata akiwa amepotea.

Msichana huyo alikuwa amepatikana katika steji ya matatu ya Naromoru alikoachwa akiwa anaelekea kumtembelea mjomba wake mjini Nanyuki kutoka mji wa Nyeri.

Alipokewa na maafisa wawili wa kiume kituoni mwendo wa saa mbili usiku lakini keshoye, mwendo wa saa kumi na moja asubuhi, Wachira akaondoka naye akidai anampeleka kituo cha kuabiri matatu ili arudi Nyeri.

“Uchunguzi wa kwanza unaonyesha afisa huyo alimpeleka nyumbani kwake ndani ya kambi ya polisi ambako alimnajisi. Baadaye alimpeleka steji na akampandisha matatu ya kuelekea Nyeri,” ripoti ikasema.

Ni katika matatu hiyo ambapo msichana alieleza wasafiri masaibu yake ndiposa wakampeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nyeri ambapo kisa hicho kiliripotiwa, kisha mshukiwa akakamatwa.

Kamanda wa polisi eneo la Kati, Patrick Lumumba jana alithibitisha hayo, na kusema kesi imewasilishwa kwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ili kufanyiwa upelelezi zaidi.

Alhamisi iliyopita, msichana wa miaka 15 katika Kaunti ya Kilifi aliripotiwa kupelekwa na wazazi wake katika kituo cha polisi kwa madai ya wizi na utundu ili ashike adabu, lakini polisi akamnajisi.

Kamanda wa Polisi Kilifi Kaskazini, Bw Njoroge Ngigi, alisema wameanzisha uchunguzi kuhusu madai hayo.

Katika Kaunti ya Migori, polisi walikuwa wanamsaka afisa wa polisi ambaye binti yake wa miaka 12, alimripoti kwa kumnajisi kisha kumfungia katika seli ya Kituo cha Polisi cha Isebania.

Habairi zilisema polisi huyo alimnajisi mtoto wake Novemba 1 na akasaidiwa na maafisa wenzake kuficha kisa hicho ambacho Mkuu wa Polisi wa Kuria Magharibi, Benard Muriuki alithibitisha kinaendelea kuchunguzwa.

Mtoto huyo ambaye alikuwa akiishi na nyanyake. alikuwa ameenda kwa babake kuchukua karo ya shule wakati alipotendewa unyama huo.

Alipohojiwa, alisema wakati alipopiga ripoti katika kituo kidogo cha polisi cha Nyabohanse, kuna afisa wa polisi wa kike ambaye alimwita babake na chifu kisha wakajaribu kumshawishi amsamehe.

Wiki hiyo hiyo Jumanne, Konstebo Kelvin Muturi anayehudumu katika Kituo cha Polisi cha Rangwe alikamatwa kwa kushukiwa kumnajisi msichana wa miaka 15 wa Kidato cha Kwanza.

“Wakati mshukiwa alipokuwa katika zamu ya usiku, inaaminika aliingia katika seli ambayo msichana alikuwepo, kisha akamfungulia na kumpeleka nyumbani kwake ambapo inashukiwa alimnajisi kabla ya kumwambia arudi katika seli,” alisema Mkuu wa DCI Kaunti ya Homa Bay, Bw Daniel Wachira.

Katika Kaunti ya Mombasa, msichana wa miaka 16 alisimulia jinsi alivyotekwa nyara na kunajisiwa na maafisa wawili wa polisi eneo la Nyali.

Msichana huyo alisema alikuwa akielekea kwa nyanyake wakati polisi walipomwamuru kuingia katika gari lao, wakamtishia kwa bastola kisha wakampeleka ufuoni ambako walimtendea unyama.

Ripoti ya NICHOLAS KOMU, IAN BYRON, AMINA WAKO na VALENTINE OBARA