Habari

Polisi majambazi

November 3rd, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA

WAKENYA wana kila sababu ya kuhofia uhai na usalama wao kwa jumla baada ya kuibuka kuwa magenge ya wahalifu yanayowahangaisha yanahusisha maafisa wa polisi.

Baadhi ya maafisa waliopatiwa mafunzo kuwalinda raia, wanatumia mafunzo hayo kuongoza magenge ya majambazi na wanakodiwa kutekeleza mauaji au kukodisha silaha zao kutumiwa na majambazi kuiba na kuua Wakenya.

Hali ni mbaya hivi kwamba maafisa hao wamekuwa na ujasiri wa kukaidi maagizo ya wakubwa wao kinyume na kanuni za kikosi cha polisi.

Katika kisa cha hivi punde, afisa wa kikosi cha kukabiliana na fujo (GSU), Anthony Kilonzo, alikamatwa na anazuiliwa na polisi, ili uchunguzi uendelee kuhusu kukiri kwake mahakamani kwamba alilipwa kutekeleza mauaji eneo la Katani.

Polisi walisema kwamba alikuwa mwanachama wa genge la majambazi wakiwemo maafisa wa usalama waliokuwa wakihangaisha wakazi wa Katani na maeneo yaliyo karibu.

Ilibainika kuwa haikuwa mara ya kwanza kwa afisa huyo kutekeleza mauaji. Alihusishwa na mauaji ya afisa wa polisi katika uwanja wa ndege wa Wilson mapema mwaka 2019.

Aidha, polisi waligundua kuwa alikuwa amesajili vijana raia katika genge lake la majambazi na kuwapa silaha hatari.

Mmoja wao aliuawa kwenye ufyatulianaji wa risasi na wapelelezi mtaani humo mapema wiki huu na silaha hatari zikapatikana.

Wiki jana, maafisa wa upelelezi walimkamata afisa wa polisi mtaani Mihango, Embakasi ambaye amekuwa akihusishwa na visa vya wizi.

Afisa huyo, David Odhiambo, alikuwa kiongozi wa genge la majambazi ambao wapelelezi walihusisha na visa vya uhalifu nchini. Sare kadhaa za polisi zilipatikana katika nyumba yake.

Polisi pia walipata risasi 30, jaketi mbili za kukinga risasi, vitambulisho vya kitaifa, leseni za kuendesha gari, noti feki za thamani ya Sh29,000 na dola za Amerika 8,800 na vitabu kadhaa vya rekodi za polisi, ishara kwamba afisa huyo alikuwa akishiriki uhalifu kwa muda mrefu.

Wizi Eastleigh

Mapema Oktoba 2019 maafisa wa idara ya upelelezi waliwakamata maafisa watano wa polisi waliohushishwa na wizi wa Sh6 milioni kutoka kwa wafanyabiashara wawili katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi.

Wao ni Simon Mwaniki, Catherine Waithera Wairimu wa vyeo vya konstebo na Wilson Cheruiyot, Daniel Kiokorir na Alex Kandie wa cheo cha koplo. Maafisa hao wote wanahudumu katika kituo cha polisi cha Kayole, Nairobi.

Inadaiwa walitekeleza wizi huo kwa ushirikiano na raia mmoja wa Cameroon, Esome Baptist na Bi Petronila Njeri Ngaara ambaye ni mhudumu katika duka lililo kituo cha polisi cha Kayole.Katika kisa kingine kilichotokea mwezi Septemba 2019,

Afisa mmoja wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) na maafisa watatu wa polisi wa utwala (AP) walikamatwa kuhusiana na wizi wa Sh72 milioni katika mtambo wa ATM wa Benki ya StanChart katika mtaa wa Nairobi West.

Maafisa wa DCI walisema waliwakamata AP hao Simon Gachuhi Karuku na mkewe Carolini Njeri Waithira katika eneo la Thogoto, kaunti ya Kiambu. Baada ya kuhojiwa, wawili hao waliwaelekeza polisi nyumbani kwa dadake Karuku, Wangari Karuku, ambaye ni afisa wa KDF katika kambi ya jeshi ya Kahawa, ambaye walimkabidhi pesa walizoiba.

Naye Wangari aliwaelekeza maafisa hao wa DCI kwa Bi Florence Wanjiru Karuku, ambaye pia ni afisa wa AP.

Mapema mwaka 2019 wapelelezi kutoka kitengo cha polisi wa kupambana na wahalifu sugu (SCPU) walipewa wajibu wa kumsaka afisa wa polisi wa Kiambu kwa tuhuma za kukodi bunduki yake kwa wahalifu.

Afisa huyo wa cheo cha Sajini Mkuu katika Kituo cha Polisi cha Kiambu alitoweka saa chache baada ya majambazi wawili kuuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Viwandani Nairobi na batola mbili zikapatikana.