Habari Mseto

Polisi motoni katika kesi ya kifo cha Samuel Wanjiru

September 23rd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi aliyepiga picha za maiti ya bingwa wa mbio za Marathon marehemu Samuel Wanjiru alijipata taabani aliposhindwa kuelezea sababu ya kupinga picha duni.

Hakimu mkuu Francis Andayi , anayepokea ushahidi kubaini kilichopelekea kifo cha Wanjiru alimhoji kwa muda mrefu sababu ya kupiga picha sisizosimulia na kuonyesha utaratibu mwafaka.

“Mtu akitazama picha hizi hawezi kung’amua chochote kuhusu kifo cha Samuel. Ukizitazama picha hizi unapasa kuona majeraha kwenye mwili wa marehemu,” alisema Andayi.

Hakimu aliongeza kusema picha hizo ziko na giza na kamwe hazifuatanishi jinsi matukio yalitokea nyumbani kwake Nyahururu alikofariki Mei 2011.

Ilibidi hakimu amwamuru shahidi huyo atoke kizimbani aonyeshe mahakama jinsi nyumba ya Wanjiru ilivyokuwa imejengwa na kule alipiga picha.

Mahakama ilifahamishwa na afisa huyo wa polisi alipoonyeshwa mwili wa Samuel ulikuwa na unadodokwa na damu puani na mdomoni.

Mama yake bingwa wa marathon Samuel Wanjiru, Hannah akiwa mahakamani Septemba 23, 2019. Picha/ Richard Munguti

Sajini Kosgey alimfanya mama yake Samuel kusononeka na kushangaa jinsi alivyopiga picha duni.

Mama huyo wa marehemu aliduwaa huku akimsikiza afisa huyo wa polisi akipepetwa na maswali mazito na Bw Andayi.

Akihojiwa na wakili Muendo Uvyu wa familia ya Samuel Wanjiru, Sajini Kosgey alisema hakuona majeraha yoyote katika sehemu ya nyuma ya kichwa cha marehemu.

“Dkt Moses Njue, aliyekuwa mkuu wa idara ya upasuaji maiti ya Serikali aliambia hii mahakama alipotoa ushahidi kwamba Samuel Wanjiru aligongwa sehemu ya nyuma kwa chuma kisicho na makali na kuvunja fuvu la kichwa chake,” alisema Bw Uvyu.

Shahidi huyo alisema hakuona majeraha hayo.Ushahidi unaendelea kutolewa huku kiongozi wa mashtaka Angela Fuchaka akisema kumesalia mashahidi sita.

Kesi itandelea Jumanne.