Habari Mseto

Polisi motoni kumumunya mamilioni ya bima wakidai walikatwa mikono na miguu

December 4th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wa polisi wa utawala waliopokea Sh2.4milioni kwa kudanganya kampuni ya bima kwamba walikatwa miguu na mikono kwenye ajali wameshtakiwa katika Mahakama ya Milimani Nairobi.

Konstebo Dominic Lusweti Masengeli na David Ichere Maina walishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Peter Ooko.

Walikanusha mashtaka 12 ya upokeaji pesa kwa njia ya udanganyifu na kughushi stakabadhi kuhusu ajali hiyo.

Konst Masengeli aliwakilishwa na wakili Bryan Khaemba, aliyestaafu mwaka huu kazi ya uhakimu.

Bw Khaemba alikuwa anahudumu katika mahakama ya Kiambu. Aliomba aachiliwe kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu.

Bw Khaemba alimsihi hakimu atilie maanani kuwa mshtakiwa huyo ni afisa wa polisi asiye na cheo, yeye ni ni Konstebo tu na mshahara wake ni mdogo.

“Mshtakiwa huyu yuko katika kile kiwango cha maafisa wa polisi wasio na cheo. Hawezi kupata dhamana inayozidi Sh100,000,” alisema Bw Khaemba.

Wakili huyo aliomba mahakama itumie mamlaka yake ipasavyo na kuwaachilia kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu.’

Mahakama iliwaachilia washtakiwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh500,000 kila mmoja na kuamuru kesi isikizwe Machi 16, 2020.

Kesi itatajwa Desemba 17 2019 upande wa mashtaka ueleze ikiwa umewakabithi washtakiwa nakala za ushahidi.

Shtaka la kwanza dhidi ya washtakiwa lilisema kati ya Septemba 22 2018 na Septemba 5 2019 walifanya njama za kuibia kampuni ya Bima ya Pioneer Sh2,440,320.

Shtaka la pili lilisema mnamo Septemba 5,2019 alipokea kutoka kwa kampuni ya Bima ya Pioneer Sh2,440,320.

Shtaka lilisema washtakiwa hao walidanganya Masengele alipata majeraha mabaya katika ajali iliyotokea kaunti ya Kitui.

Mahakama ilifahamishwa wawili hao waligushi ujumbe wa polisi kuhusu ajali hiyo ulipeperushwa na Kamanda wa Polisi eneo la Mwingi.

Hakimu alifahamishwa mnamo Julai 10 2019 katika afisi za kampuni ya Bima ya Pioneer Assurance barabara ya Harambee wakiwa na nia ya kulaghai walipeana ujumbe feki kuhusu ajali hiyo kwa Bi Irene Njagi wakidai umetayarishwa na kamanda huyo.

Pia walishtakiwa kwa makosa ya kujitengenezea cheti cha ajali Ref:P/AL807/0004550 wakidai kimetayarishwa na Idara ya Polisi.