Polisi motoni kwa msongamano wa magari wikendi

Polisi motoni kwa msongamano wa magari wikendi

Na MWANDISHI WETU

POLISI wametwikwa lawama kuhusiana na msongamano mkubwa ulioshuhudiwa katika barabara kuu ya Thika mnamo Jumamosi ambapo wakazi wa Nairobi walilazimika kukesha barabarani baada ya kuwekewa vizuizi, tukio linaloendelea kukemewa na raia.

Wanahabari, madaktari na madereva wa ambulensi ambao walikuwa wakiwakimbiza wagonjwa hospitalini ni kati ya watu wanaotoa huduma spesheli na wana vibali maalum, ambao walizuiwa kupita kwenye vizuizi vilivyowekwa na polisi katika barabara hiyo yenye shughuli nyingi.

Kudhihirisha ukatili wa polisi, Afisa Mkuu wa Polisi eneo la Kasarani Peter Nyaga aliwaamrisha maafisa wake kutoruhusu gari lolote kupita vizuizi vilivyowekwa huku baadhi wakiwasukuma waliojaribu kujadiliana nao ndani ya magari yao.

“Usituambie jinsi tunavyofaa kufanya kazi yetu,” Bw Nyaga alieleza Taifa Leo alipoulizwa kwa nini hakuwa akiwaruhusu watu wenye vibali kupita vizuizi vilivyowekwa.

Imebainika kwamba, polisi walikuwa wameshikilia kwamba wote waliokuwa kwenye msongamano huo wangelala barabara isingekuwa ni dereva mmoja wa ambulensi ambaye alikuwa amebeba mama mwenye mtoto mdogo mgonjwa kutembea kilomita moja ili kuwashawishi wamruhusu amkimbize hospitalini.

Mama huyo alikuwa amembeba mwanawe aliyekuwa katika hali mbaya kwa zaidi saa mbili katika msongamano huo na aliathirika vibaya kisaikolojia kiasi cha kutotamka neno kwa wanahabari, ambulensi hiyo ilipopishwa.

Polisi hawakuwa na budi kupisha ambulensi hiyo kwa kuruhusu magari yaliyokuwa mbele yake kupita hata baada ya baadhi ya waendeshaji magari kukubali kusalia barabarani mradi tu ambulensi hiyo ipite.

Kama kwamba hayo hayatoshi, polisi waliweka vizuizi tena baada ya ambulensi kupita na kuzidisha msongamano zaidi huku waliokwama barabarani wakipiga nduru na kulalamikia udhalimu huo.

Hata wanahabari wa Taifa Leo waliojaribu kufuata ambulensi hiyo ili kuthibitisha kwamba mama huyo amepata msaada hospitalini walizuiwa huku polisi wakisema hawakuwa wakitambua vibali hivyo.

Hata hivyo, Bw Nyaga alikataa kuelezea kwa nini vizuizi hivyo viliwekwa ghafla bila utaratibu maalum wa kuhakikisha wanaotoa huduma spesheli na wana vibali wanaruhusiwa kuendelea na safari yao.

Pia maswali yameibuka ni nani huwa anatoa amri katika idara ya polisi kutokana na visa vinavyoendelea kukithiri vya maafisa hao wa usalama kuwadhulumu raia na jinsi ambavyo oparesheni za kafyu huendeshwa.

Licha ya Wizara ya Usalama wa Ndani kutoa taarifa kwamba msongamano barabarani utaangaziwa na polisi wa trafiki kuhakikisha wasafiri wanaendelea na safari yao, polisi mnamo Jumapili usiku walirudia kitendo cha Jumamosi kwa kuwazuia wenye magari barabarani.

You can share this post!

Caf haijapata mwandalizi wa fainali za AWCL

UDA yaanza kuwasajili wanachama mashinani katika jamii za...