Habari

Polisi mwanamke apatikana amefariki katika nyumba yake mtaani Umoja

May 25th, 2019 1 min read

Na NYABOGA KIAGE

AFISA wa polisi wa kike ambaye amekuwa akihudumu katika kituo cha polisi cha bungeni alipatikana Ijumaa katika nyumba yake mtaani Umoja, Nairobi akiwa amefariki.

Polisi wamesema Konstebo Hellen Kwamboka baada ya kuondoka kazini Alhamisi saa moja jioni, alikosa kuingia kazini Ijumaa na hivyo msako ukaanzishwa.

Walilazimika kuingia nyumbani kwake na hapo wakakuta mwili wake, huku kukiwa na damu iliyomwagika kote na ambapo kulikuwa na majeraha kichwani.

Polisi wamesema huenda mwendazake alinyongwa kwa sababu kulikuwa na alama shingoni.

Maafisa akiwemo afisa wa Uchunguzi wa Jinai eneo la Buruburu na maafisa wengine kutoka Idara ya Uchunguzi wa Jinai walifika eneo la tukio.

Ripoti ya maafisa inasema mlango wa kuingia katika nyumba ya marehemu Kwamboka ulikuwa umefungwa kwa ndani.

“Maafisa walipogundua mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani, walibainisha mambo hayakuwa mazuri,” ripoti imesema.

“Hakuna kifaa chochote cha maangamizi kilipatikana hapo…. Inashukiwa mpenzi wake wa kiume aliyemtembelea Alhamisi alimuua na kisha akatoroka.”

Maafisa pia wamesema simu ya Kwamboka ilikuwa imetoweka kukiwa na uwezekano “iliibwa na kuzimwa.”

Mwili umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Chiromo.