Habari

Polisi Nakuru wawasaka wahalifu wawili waliotoroka wakiwa na majeraha ya risasi

December 8th, 2020 1 min read

Na RICHARD MAOSI

POLISI kutoka Nakuru wanaendelea kutafuta wahalifu wawili waliotoroka na majeraha ya risasi baada ya wenzao sita kuuawa.

Makabiliano hayo makali baina ya wahalifu waliojihami na polisi yalitokea Jumatatu jioni katika mzunguko wa Setion 58, kilomita mbili hivi kutoka mjini Nakuru na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.

Katika operesheni hiyo kali polisi walinasa pingu, bastola, risasi, simu ya polisi na mikoba.

Akizungumza na Taifa Leo Afisa wa idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) Antony Sunguti alisema wanane hao walikuwa wanapanga kutekeleza uhalifu mjini Nakuru.

Polisi wakikagua gari na silaha za wahalifu sita waliouawa katika mzunguko wa Section 58 Nakuru, Jumatatu jioni. Picha/ Richard Maosi

Kulingana na Sunguti, maafisa wa DCI waliwafuatilia kupitia maongezi ya simu na huenda gari walilokuwa wakitumia kutekeleza uhalifu lilikuwa limeibiwa kutoka jijini Nairobi

Alieleza kuwa afisa mmoja wa polisi pia alipata majeraha ya risasi katika patashika hiyo.

Wahalifu hao ambao inakisiwa walikuwa wakitoka jijini Nairobi, walikataa kusimama walipokaribia mjini Nakuru na hapo wakaanza kuwafyatulia polisi risasi.

“Hata hivyo walilemewa na polisi ndiposa gari lao aina ya Probox likatumbukia ndani ya mtaro, katika barabara inayounganisha Nakuru – Nyahururu,”akasema.

Makabiliano hayo makali yalisimamisha shughuli za usafiri huku baadhi ya wapita njia na waendeshaji bodaboda wakikimbilia usalama wao.

Polisi wameanzisha uchunguzi wa kina kubaini asili ya majambazi hao sita waliowawa pamoja na wengine wawili ambao walitoroka.

“Tunaomba raia kutoa taarifa muhimu ambazo zitawasaidia polisi kuwatia nguvuni magenge ya wahalifu,” akasema.