Habari Mseto

Polisi ndani baada ya kunaswa wakiiba Heroin ya Sh75 milioni

March 10th, 2019 2 min read

BERNARDINE MUTANU na BENSON MATHEKA

MAAFISA wa polisi walikamatwa Jumamosi na makachero kwa kujaribu kuiba dawa za kulevya za thamani ya Sh75 milioni.

Dawa hizo zilikuwa zikisafirishwa na kulingana na DCI, na maafisa hao walinaswa na kamera za CCTV katika kisa hicho.

“Afisa mmoja alikamatwa Ijumaa mwingine Jumamosi. Wote wamezuiliwa ili tukamilishe uchunguzi,” alisema Khamisi Masa, kutoka shirika la kukabiliana na mihadarati.

Huenda wawili hao, pamoja na washukiwa wengine katika kisa hicho wakafikishwa mahakamani Jumatatu, alisema, bila kutoa habari kuhusiana na zilikokuwa zikipelekwa.

Kulingana na taarifa ya Idara ya Upelelezi wa Jinai ( (DCI), maafisa hao (Koplo Alloys Onyango na Konstebo Arbanus Mutunga) waliwashawishi walanguzi wa dawa za kulevya na wamiliki wa kilo hizo 25 za heroin na kuiba licha ya kuwa zilikuwa zimekamatwa.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa maafisa hao walitumia mlanguzi wa dawa za kulevya Peter Okoth Odongo ili kuwashawishi wamiliki wa dawa hizo, Alfric Odhiambo Otieno na Kenneth Sinzore na baada ya kuchukua dawa hizo wakawatupa washukiwa hao.

“Hakuna atakayesazwa katika vita dhidi ya uhalifu,” ilisema afisi ya DCI kuhusiana na kisa hicho.

Kisa hicho kilitokea saa kadhaa baada ya makachero hao kumkamata afisa mwenye cheo cha Inspekta Mkuu wa Polisi na watu wengine watatu kwa madai ya kupokea hongo ya Sh2 milioni.

DCI ilisema kwenye akaunti yake ya Twitter kwamba Inspekta Mkuu wa Polisi Kennedy Omondi, Stanilus Otieno, Eddie Obwaka na Boniface Omengi walikuwa wakijifanya maafisa wa idara ya uhamiaji na kutaka kuhongwa ili kuachilia pasipoti na stakabadhi zingine za waathiriwa.

“Kukamatwa kwao kulifuatia ripoti ambayo walalamishi walipiga kwa polisi baada ya paspoti zao na stakabadhi zingine kutwaliwa na watu hao waliojifanya maafisa wa Idara ya Uhamiaji,” ilisema DCI katika ujumbe huo.

Afisa huyo pamoja na wenzake waliitisha hongo ya Sh10 milioni na walikamatwa walipokuwa wamefika kupokea Sh2 milioni.

Kati ya wanne, wawili walitoroka wakati wa kisa hicho ambapo makachero hao walipata bastola na risasi kutoka kwa washukiwa hao.