Habari Mseto

Polisi pabaya kwa mauaji ya mwanamke City Park

June 13th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAAFISA wawili wa Polisi wa Utawala walishtakiwa Jumatatu kwa mauaji ya mwanamke aliyekuwa na mwanamme ndani ya gari katika bustani ya City Park kaunti ya Nairobi mwezi uliopita.

Mauaji ya Bi Jane Wangui Waiyaki mwenye umri wa miaka 41 yalizua hisia kali huku miito ikitolewa kwenye vyombo vikuu vya habari na mitandao ya kijamii kwamba waliohusika watiwe nguvuni na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Konstebo Kipkorir Chirchir na Godfrey Kipng’eticj Kirui walifikishwa mbele ya Jaji James Wakiaga na kushtakiwa kwa mauaji ya Jane mnamo Mei 20, 2018.

Shtaka lilisema wawili hao walimuua Jane katika bustani akiwa ndani ya gari na Bernard Chege mwenye umri wa miaka 26.

Konstebo Chirchir na Konstebo Kirui walikanusha shtaka dhidi yao.

Wakili Ham Langat anayewatetea aliomba waachiliwe kwa dhamana akisema “ ni haki yao kwa mujibu wa Kifungu 49 (1)(H).”

“Dhamana ni haki ya kila mshukiwa anayeshtakiwa hata kama anakabiliwa na kosa gani,” Bw Langat alimweleza Jaji Wakiaga.

Aliomba mahakama itumie mamlaka yake kuwaachilia kwa dhamana washtakiwa aliosema ni maafisa wa polisi.

“Washtakiwa ni watumishi wa umma. Waliposhikwa walikuwa wakiendelea na kazi yao ya kudumisha amani. Washukiwa hawa walikuwa wameenda katika eneo la bustan ya City Park kutekeleza kazi yao baada ya taarifa kuwa kungelikuwa na shambulizi la kigaidi kwenye majengo ya Serikali na pia hospitali ya Aga Khan,” alisema Bw Langat.

Wakili huyo aliomba korti iwaachilie kwa dhamana wafanye kesi wakiwa nje.

Kiongozi wa mashtaka Bi Catherine Mwaniki alipinga ombi hilo akisema kuwa washtakiwa watatoroka wakiachiliwa kwa dhamana.

“Nahitaji muda niwasilishe taarifa kutoka kwa afisa anayechunguza kesi hii akisimulia sababu za kupinga kuachiliwa kwa maafisa hawa wawili wa polisi kwa dhamana,” alisema Bu Mwaniki.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kuwa atahitaji ripoti kutoka kwa jamii ya marehemu  endapo wangelipendelea washtakiwa wakiachiliwa kwa dhamana.

“Ripoti ya familia ya marehemu yahitaji kuwasilishwa mbele ya hii korti. Pia ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia kuwahusu washukiwa hawa yahitajika,” alisema Bi Mwaniki

Mahakama ilifahamishwa marehemu aliwaacha watoto watatu wandogo.

Jaji Wakiaga alikataa ombi la Bw Langat la kuwataka washtakiwa wazuiliwe katika kituo cha polisi.

Alisema kwa vile wamekanusha shtaka “pale wanaweza kuzuiliwa kwa sasa ni gereza la Viwandani.”

Aliamuru ombi ladhamana lisikizwe mnamo Juni 19 2018. Alimwagiza Bi Mwaniki amkabidhi Bw Langat ripoti ya familia ya mhasiriwa pamoja na afidaviti ya afisa anayechunguza kesi hiyo aone ikiwa kuna majibu anayoweza kutoa.