Polisi sasa kumfungulia shtaka mwanamume aliyeua watu  8

Polisi sasa kumfungulia shtaka mwanamume aliyeua watu 8

NA MERCY KOSKEY

POLISI mjini Nakuru wamesema watamfungulia Moses Kipchirchir shtaka moja licha ya kukiri kuua takribani watu wanane ndani ya miaka 10 iliyopita.

Kulingana na mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) wa Mogotio, Bw Lucas Tumbo, mshukiwa huyo atashtakiwa na mauaji ya Veronicah Kanini aliyekuwa mfanyabiashara mjini Nakuru; ambaye Kipchirchir alikiri kumuua na kumzika.

Bi Kanini aliondoka nyumbani kwake mtaa wa Mawanga mjini Nakuru na hakurejea jioni hiyo baada ya kazi.

Mumewe, Bw Mariko Njuguna alipiga ripoti kwa kituo cha polisi cha Central kabla ya kuelekezwa Mogotio aliposaidika kumpata mshukiwa kujua kilichojiri kwa mkewe siku 11 baadaye.

Bw Tumbo alielezea kuwa itawalazimu kutuma faili za Bi Purity Chebet (mkewe Bw Kipchirchir) na mwanawe wa miezi kumi na minane, ambao pia alikiri kuwaua, kwa afisi ya mashtaka ya umma kwa maelekezo kabla ya kumshtaki na mauaji mengine aliyokiri kuyatekeleza.

“Pindi tu majibu ya DNA yatawasilishwa kwetu kutoka kwa mtaalamu wa maabara Kaunti ya Kisumu, tutazikusanya na kuzituma kwa afisi za mkuu wa mashtaka ya umma ili Bw Kipchirchir ashtakiwe,” alisema Bw Tumbo.

Bw Tumbo aliongeza kuwa pia walituma faili ya kesi ya mauaji ya Bw Samuel Njoroge, ambaye Bw Kipchirchir alikiri kumuua na kumzika 2012 kwa mkuu wa upelelezi Molo kwa uchunguzi zaidi kabla ya kushtakiwa.

Mnamo Desemba 29, mwaka jana, Bw Kipchirchir alielekeza maafisa kwa msitu wa Kiptunga ambapo alidai kumzika Bw Njoroge.

Alikiri kuwa mnamo 2012, akifanya kazi ya kuchoma makaa alimuua mwathiriwa kwa shokakabla ya kumzika akidai alimuua afisa huyo wa misitu alipomkabili kwa kuendesha shughuli haramu msituni na pia kukataa kuchukua hongo ya Sh1,200.

Uchunguzi wa mabaki ya mwili wa Bi Chebet na mwanawe katika makafani ya Nakuru ulionyesha kuwa walifariki kwa kunyongwa.

Kwa sasa Bw Chirchir atasalia rumande kwenye gereza la Nakuru kabla ya kufikishwa katika mahakama ya Kabarnet Jumatatu.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Rais afaa kutatua tatizo la wakulima wa...

Hofu kaunti zikiweka dawa zilizopitwa na muda wa matumizi...

T L