Habari za Kitaifa

Polisi shujaa aliyesombwa na mafuriko akiokoa raia Muthurwa bado hajapatikana

April 7th, 2024 2 min read

Na MERCY KOSKEI

FAMILIA ya polisi aliyesombwa na mafuriko jijini Nairobi baada ya mvua kubwa kunyesha, inaitaka serikali kuongeza juhudi za kumtafuta ili kupata mwili wake.

Konstebo David Kibet Chesire, aliyekuwa akihudumu katika Kituo cha Polisi cha Kamukunji, jijini Nairobi, alisombwa na mafuriko mnamo Machi 24, alipokuwa akijaribu kuiokoa familia iliyokuwa imezingirwa na maji.

Alikanyaga kwenye sehemu iliyokuwa na shimo kubwa na kutumbukia ndani, na juhudi za kuupata mwili wake hazijafaulu tangu wakati huo.

Bunduki yake aina ya AK47, iliyokuwa na risasi 30 pia haijapatikana.

Polisi huyo alikuwa ameandamana na askari wenzake, walipowapata wanawake watatu na mtoto mmoja wakiwa wamekwama kwenye kibanda kilichokuwa kimebomoka upande mmoja.

Kwenye kisa hicho kilichofanyika mwendo wa saa nne usiku, polisi hao walichukua hatua za haraka na kuwaokoa wanne hao.

Hata hivyo, Konstebo Chesire alirudi karibu na vibanda hivyo wakati upande uliobaki ulibomoka, hilo lilimfanya kusombwa na mafuriko.

Nyumbani kwao eneo la Kampi ya Moto, Rongai, Kaunti ya Nakuru, jamaa na marafiki wake walikusanyika kwa maombi wakiwa na matumaini ya kuupata mwili wa Bw Chesire.

Wana matumaini ya kuupata mwili wake na kumfanyia mazishi ya heshima kutokana na kitendo chake cha kishujaa.

Kulingana na mamake, Bi Elizabeth Murugi, habari kuhusu ajali ya mwanawe zilikuwa za kuhofisha. Zaidi ya hayo, kutopatikana kwa mwili wake kumeleta hali ya mahangaiko ya kimawazo kwa familia hiyo kwa muda wa wiki mbili zilizopita.

Alisema kuwa maombi ya familia hiyo ni mwili wa Bw Kibet uweze kupatikana ili afanyiwe mazishi yanayofaa. Hili ni ikizingatiwa alifariki kama shujaa akiwa kazini, akijaribu kuokoa maisha ya watu wengine.

Babake Joseph Chesire

Babake, Joseph Chesire, amekuwa katika eneo la mkasa kwa zaidi ya wiki mbili, akitumaini kwamba mwili wa mwanawe utapatikana na familia hiyo kukabidhiwa ili wamwandalie mazishi.

Familia hiyo inahisi kwamba, serikali imekuwa ikilegea katika kutoa usaidizi ufaao kwa njia ya raslimali na vifaa vinavyofaa, kwenye juhudi za kuutafuta mwili huo.

Wanasema kuwa serikali inafaa kuheshimu maisha na kujitolea kwake, kwa kufanya kila iwezalo kuupata mwili wake na kumwandalia mazishi yanayofaa.

“Alifariki akiwa kazini. Ninairai serikali kutusaidia. Haifai kuchoka kwenye juhudi za kuutafuta mwili wake,” akasema Bi Murugi.

Bi Murugi alipata habari kuhusu mwanawe wa kwanza Jumatatu asubuhi. Mumewe aliambiwa Kibet alikuwa amejeruhiwa na alikuwa katika hali mahututi. Aliambiwa asafiri hadi jijini Nairobi.

Bw Chesire, alilazimika kuacha kwenda katika shamba lake na badala yake kurudi nyumbani mwake na kuelekea jijini Nairobi.

Aliambiwa mwanawe amefariki

Baadaye, aliambiwa mwanawe alikuwa ashafariki.

“Wakati aliniambia kuhusu yale yaliyofanyika, nilishangaa sana. Nilianza kutetemeka. Niliambia Mungu kunipa nguvu, huku mume wangu akielekea Nairobi ili kupata maelezo kamili kuhusu yaliyofanyika. Nilitarajia kupata habari nzuri, lakini niliambiwa alikuwa ashafariki,” akasema mamake Chesire.

Kulingana na Bi Murugi, alizungumza mara ya mwisho na mwanawe saa tatu usiku Jumapili, wakati alimpigia babake kuwajulia hali.

Bi Murugi alisema Bw Kibet alikuwa mchangamfu. Alisema aliwaahidi kuwatembelea Jumamosi, Machi 31, japo hilo halikutimia.

Kibet ana umri wa miaka 33 na watoto wawili; mmoja wa miaka minne na mwingine wa miaka tisa.

Alijiunga na Idara ya Polisi mnamo 2017 baada ya kufuzu kutoka Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Embakasi.