Habari

Polisi shujaa wa Westgate aaga dunia

June 16th, 2024 1 min read

STEVE OTIENO na NYABOGA KIAGE

AFISA wa zamani wa polisi aliyepata umaarufu kwa kupambana na wahalifu na kuwaokoa wengi katika shambulio la Westgate Mall mnamo 2013, aliaga dunia wikendi.

Stephen Lelei, ambaye alishikilia cheo cha inspekta, aliaga dunia katika Hospitali ya Kiambu baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Wanafamilia wake walisema siku za mwisho za uhai wake, alionekana mnyonge na kusumbuliwa.

Wengine pia walisema alikuwa na msongo wa mawazo hali ambayo ilidhoofisha zaidi afya yake.

Bw Lelei alipanda ngazi katika idara ya polisi na kuwa kamanda wa vituo mbalimbali vya polisi Nairobi na Machakos.

Kati ya vituo hivyo ni Kabete, Pangani, Mlolongo na Soweto.

Alikuwa kati ya maafisa tisa ambao walienziwa sana na serikali wakati wa shambulio la Westgate 2013.

Wakati huo, alikuwa kamanda wa kituo cha polisi cha Kabete.

Kutokana na weledi wake na polisi wengine wanane, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alimtunuku kwa tuzo ya hadhi inayofahamika kama Silver Star.