Polisi sita wakana kuua ndugu wawili Embu agosti 1, 2021

Polisi sita wakana kuua ndugu wawili Embu agosti 1, 2021

Na RICHARD MUNGUTI

JITIHADA za maafisa sita wa polisi za kupinga wasishtakiwe kwa mauaji ya ndugu wawili kaunti ya Embu Agosti 1 2021 ziligonga mwamba jana mahakama kuu ilipotupilia mbali maombi matatu ya kufutilia mbali kesi hiyo.

Akikataa ombi la maafisa hao sita kupinga wasifunguliwe mashtaka ya mauaji ya Emmanuel Mutura Ndwiga na Benson Njiru, Jaji Daniel Ogembo alisema suala la vifo vya wavulana hao lina uzito wa kitaifa na limetega hisia za wananchi wote.Jaji Ogembo alisema lazima haki itendeke na endapo washtakiwa hao wako na ushahidi hawakuhusika na mauaji ya ndugu hao, bila shaka mahakama itawaachilia huru.

Jaji huyo alisema tangu Agosti 14, 2021 maafisa hao waliwasilisha maombi matatu ya kupinga wakishtakiwa kwa mauaji ya Njiru na Mutura, na badala yake mahakama iamuru uchunguzi wa kubaini kilichosababisha vifo hivyo.

Maafisa hao wa polisi Koplo Corporal Benson Mbuthia Mabuuri, Koplo Consolata Njeri Kariuki,Martin Musamali Wanyama, Nicholas Sang Cheruiyot, Lilian Cherono Chemuna na James Mwaniki Njohu waliwasilisha maombi matatu mbele ya Jaji Ogembo na Jaji Weldon Korir wakiomba kushtakiwa kwao kwa mauaji kupigwe breki, mahakama kuu iamue ikiwa uchunguzi wa kubaini kilichosababisha vifo vya Mutura na Njiru utolewe.

Katika maombi yao washtakiwa hao walisema Kifungu cha Katiba  nambari 276 na sheria nambari 386 na 387 ya sheria za uhalifu sita hao zimeipa mahakama kuu uwezo kuamua ikiwa kesi ya mauaji itaendelea ama uchunguzi utafanywa kwanza kubaini kilichosababisha mmoja kuaga.

Akiwasilisha maombi yao wakili Danstan Omari alimweleza Jaji Ogembo kuwa sheria nambari 386 na 387 zisema uchunguzi wa kubaini kilichosababisha kifo cha mshukiwa anayekata roho akiwa aidha mikononi mwa polisi ama mikononi kwa askari jela ama anapozuiliwa gerezani.

Katika ushahidi aliowasilisha mbele ya Majaji Ogembo na Korir, Bw Omari alisema wahasiriwa waliruka kutoka kwa gari la polisi na kuanguka na kufa papo hapo.“Sheria imetoa mwelekeo wa kufuatwa kesi kama hii inapotokea na kamwe haisemi washukiwa washtakiwe kwa mauaji mbali hakimu apokee ushahidi ndipo abaini ikiwa mashtaka ya mauaji yatafunguliwa au la,” Bw Omari.

Maombi hayo yalipingwa vikali na kiongozi wa mashtaka Bi Jacinta Nyamosi na rais wa chama cha wanasheria nchini LSK Bw Nelson Havi waliosema ombi hilo la sita hao ni mbinu ya kuchelewesha haki ikitendeka.Jaji Ogembo alikubaliana na Bi Nyamosi na Bw Havi na kuamuru washtakiwa wajibu mashtaka ya mauaji.

Washtakiwa hao walikana waliwaua wavulana hao.Waliagizwa wazuiliwe katika magereza ya Viwandani na Langata.Jaji Ogembo aliamuru ombi la washtakiwa hao la kuachiliwa kwa dhamana lisikizwe Septemba 22, 2021.

  • Tags

You can share this post!

HASLA BANDIA

Ninauza mayai ya Sh1.5m kila siku – Ruto