Polisi sita wanaohusishwa na mauaji ya ndugu wawilli wa Embu wakamatwa

Polisi sita wanaohusishwa na mauaji ya ndugu wawilli wa Embu wakamatwa

Na SAMMY WAWERU

MAAFISA sita wa polisi waliotajwa kuhusika na mauaji ya ndugu wawili Embu mapema mwezi huu wamekamatwa Jumatatu jioni na kusafirishwa hadi Nairobi wakisubiri mashtaka. 

Mamlaka Huru ya Kuchunguza na Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA), imependekeza waachishwe kazi mara moja, huku ripoti hiyo ikitarajiwa kuwasilishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) ili kufunguliwa mashtaka.

“Waachishwe kazi mara moja, kufuatia kukamilika kwa uchunguzi wa mamlaka huru na ripoti kuwasilishwa kwa DPP. Kwa sasa maafisa hao wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji. Mapendekezo haya hayatabadilika,” IPOA imeeleza kwenye taarifa.

Kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha sheria ya IPOA, mauaji yanayofanyika katika kituo cha polisi, kusababishwa na askari au mwanachama wa kikosi cha polisi (NPS), mamlaka hiyo inapaswa kuyachunguza.

“Kifungu cha 29 cha sheria za IPOA pia kinasema endapo uchunguzi unaonyesha kuna tendo la uhalifu, mapendekezo ya kufunguliwa kwa kesi ya mashtaka yawasilishwe kwa DPP.

“Uchunguzi wa mamlaka unaonyesha kuna kesi ya uhalifu kwa maafisa hao sita,” inafafanua.

Kwenye mapendekezo ya IPOA, askari waliotajwa kuhusika katika mauaji ya wavulana Benson Njiru na Emmanuel Mutura, wasalimishe silaha walizonazo mara moja.

“Maafisa na wakuu wa polisi waliohojiwa na kuandikisha taarifa washirikiane na IPOA watakapohitajika kwenye uchunguzi zaidi,” mamlaka inasema.

Mbali na kesi ya mauaji, IPOA imesema inaendelea kushughulikia mashtaka mengine ya utepetevu kazini kwa maafisa waliohusika katika mchakato mzima wa kufariki kwa wawili hao.

Vijana Njiru na Mutura walifariki mikononi mwa polisi, baada ya kukamatwa kwa madai ya kukiuka sheria za kafyu.

Walizikwa Ijumaa wiki iliyopita, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi na wanasiasa mbalimbali, wote wakishinikiza maafisa husika kuchukuliwa hatua kisheria.

You can share this post!

Corona ilivyohangaisha makahaba dhuluma zikiongezeka

Natembeya awatimua maafisa wa usalama